Jan 05, 2022 02:40 UTC
  • Kujiuzulu Waziri Mkuu Hamdok na kushitadi mgogoro wa kisiasa nchini Sudan

Abdalla Hamdok, Waziri Mkuu wa Sudan ambaye hivi karibuni alitishia kujiuzulu, hatimaye Jumapili usiku alitangaza rasmi kujiuzulu nafasi hiyo mbele ya waandishi wa habari.

Hatua ya kujiuzulu Waziri Mkuu wa Sudan imekuja kutokana na kukukithiri maandamano na upinzani wa wananchi wanaowataka majenerali wa kijeshi warejee makambini mwao na waruhusu serikali na masuala ya kisiasa ya nchi hiyo yaongozwe na raia.  Sambamba na kutangaza uamuzi wake huo, Hamdok alisema kuwa: Tumependekeza mipango kadhaa, lakini hakukuweko wa kutusikiliza. Mimi nilikuwa na uwezo wa kufanya juhudi mpaka hapa ili kuiokoa nchi na hatari ya kusambaratika na kuelekea upande wa maafa.

Waziri Mkuu wa Sudan aliyejiuzulu amesema pia kuwa: Mgogoro mkubwa wa leo katika hatua ya awali ni mgogoro wa kisiasa, lakini hali hiyo imekuwa katika mwenendo wa kubadilika na kuzikumba nyanja zote za maisha ya kiuchumi na kijamii za wananchi na hivyo kuwa mgogoro ulioenea katika sekta zote. Hamdok amebainisha kwamba, kwa kuzingatia kuendelea malalamiko na upinzani wa umma dhidi ya hatua ya wanajeshi ya kutwaa na kuhodhi madaraka, kuna haja ya kufikiwa makubaliano mapya ya kukabidhi hatamu za uongozi wa nchi.

Hii ni katika hali ambayo, katika siku za hivi karibuni, mji mkuu Khartoum na miji mingine ya Sudan imeendelea kushuhudia wimbi kubwa la maandamano ya wananchi ya kulalamikia hali ya kisiasa ya nchi hiyo na kuunga mkono kuweko serikali ya kiraia. Takwimu zinaonyesha kuwa, idadi ya watu waliouawa tangu jeshi la Sudan litwae madaraka ya nchi Oktoba 25 mwaka jana imepindukia 55.

Abdul-Fattah al-Burhan Mkuu wa Baraza la Utawala la Sudan

 

Mauaji na ukandamizaji wa karibuni kabisa uliofanywa na vikosi vya usalama vya Sudan ni ule wa Alkhamisi iliyopita ambapo waandamanaji 5 waliuliwa na wengine 300 kujeruhiwa. Jumuiya ya Wafanyakazi nchini Sudan imetangaza kuwa, yaliyotokea Alkhamisi iliyopita yalikuwa mauaji ya umati.

Kabla ya uamuzi huu wa kujiuzulu Abdalla Hamdok, kulikuwa na tetesi za kujiuzulu mwanasiasa huyu ambaye majuma machache yaliyopita pia yeye mwenyewe alinukuliwa akisema mbele ya sahkhsia wa kisiasa na kifikra kuwa, atajiuzulu wadhifa wake huo wa Waziri Mkuu wa Sudan muda si mrefu. Hata hivyo, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Abdul-Fattah al-Burhan Mkuu wa Baraza la Utawala la Sudan ambaye pia ndiye Kamanda wa Jeshi la Sudan, Hamdok alibadilisha uamuzi wake.

Abdalla Hamdok ametangaza kujiuzulu nafasi ya Waziri Mkuu wa Sudan katika hali ambayo tarehe 25 Oktoba mwaka jana 2021, jeshi la Sudan lilifanya mapinduzi mengine ya kijeshi na kuivunja serikali ya mpito ambayo ilikuwa inashirikisha pia raia. Hamdok ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa serikali hiyo naye aling'olewa madarakani na kuwekwa kizuizini.

Kabla ya kurudi tena madarakani, Hamdok alisema kuwa atachukua tena cheo cha Waziri Mkuu kama matakwa ya wananchi yataheshimiwa akisisitiza kuwa, mgogoro mkuu wa Sudan ni mvutano uliopo baina ya wanasiasa na wanajeshi.

Maandamano ya wananchi wa Sudan

 

Hamdok alirejea madarakani baada ya kufikiwa makubaliano ya kisiasa na alitishia kujiuzulu kama vifungu hivyo havitoheshimiwa. Wananchi walimtuhumu Hamdok kuwa amewasaliti lakini alikanusha na kusisitiza msimamo wake wa kujiuzulu kama wanajeshi watakataa kuheshimu matakwa ya wananchi. Inaonekana kuwa, anga ya kisiasa nchini Sudan hususan mivutano baina ya Hamdok na wanajeshi wenye satua kumeitumbukiza tena Sudan katika mkwamo wa kisiasa na hivyo kumfanya Waziri Mkuu huyo kutokuwa na chaguo ghairi ya kujiuzulu.

Kutangaza kujiuzulu Abdalla Hamdok kutoka katika wadhifa wake wa Waziri Mkuu kumeibua wasiwasi kuhusiana na mustakabali wa Sudan, nchi ambayo miaka mitatu iliyopita ilishuhudia vuguvugu la wananchi lililohitimisha miaka mingi ya utawala wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Omar Hassan al-Bashir na kisha kukaundwa serikali ya mpito. Baada ya hapo Abdalla Hamdok na afisa wa zamani wa Umoja wa Mataifa akateuliwa kuwa Waziri Mkuu kwa mujibu wa makubaliano yaliyokuwa yamefikiwa baina ya raia na wanajeshi.

Omar Hassan al-Bashir Rais wa zamani wa Sudan

 

Pamoja na hayo, katika miaka ya hivi karibuni kumeshuhudiwa hitilafu kubwa baina ya serikali ya kiraia na wanajeshi ambao wamekuwa na nafasi muhimu Baraza la Mpito na la Utawala.

Kuhusiana na hilo, Hamdok anasema: Serikali ya Mpito ilikuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ambapo muhimu zaidi ni kudorora uchumi, kutengwa kimataifa, ufisadi na mzigo wa madeni ambayo ni zaidi ya dola bilioni 60, kuvurugika sekta ya huduma za jamii, elimu, afya na matatizo katika muundo wa kijamii ambayo yaliibuka baada ya vita vya majimbo ya Darfur, Kordofan Kusini,  Blue Nile na matatizo mengine chungu nzima.

Filhali baada ya Hamdok kujiuzulu, Sudan imeingia katika hatua na marhala mpya ya mgogoro wa kisiasa na inatarabiriwa kwamba, mizozo ya kisiasa na malalamiko ya wananchi yatachukua mkondo mpya katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Tags