Jan 07, 2022 03:30 UTC
  • Maelfu ya shule zimefungwa kutokana na ugaidi Burkina Faso

Maelfu ya shule zimefungwa nchini Burkina Faso kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya magenge mbalimbali ya wabeba silaha wenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida na Daesh.

Wizara ya Elimu nchini humo imesema, kufikia Disemba 31 mwaka uliomalizika wa 2021, shule 3,280 zilikuwa zimefungwa nchini humo kutokana na hujuma za magenge hayo.

Taarifa ya wizara hiyo imeeleza kuwa, idadi hiyo ni sawa na asilimia 13 ya shule zote za nchi hiyo, na kufungwa kwa shule hizo kumewaacha wanafunzi 511,221 na walimu 14,901 katika njiapanda wasijue cha kufanya.

Msemaji wa Serikali ya Burkina Faso, Alkassoum Maiga amesema takwimu hizo mpya zinatisha na kutia wasiwasi mkubwa.

Mei mwaka jana, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilisema kufungwa kwa maelfu ya shule katika nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika kumeathiri masomo ya wanafunzi 304,450 wakiwemo 156,456 wa kiume, 147,994 wa kike, mbali na kufanya walimu 11,068 wapoteza ajira. 

Athari za hujuma za kigaidi B/Faso

Burkina Faso ambayo ni moja ya nchi maskini zaidi duniani inapambana na uasi na hujuma za makundi ya wabeba silaha  ambayo yalikimbilia nchini humo mwaka 2015 kutokea katika nchi jirani ya Mali.

Makundi hayo ya kigaidi yamekuwa yakivizia misafara barabarani, kutega mabomu kando ya barabara na kutekeleza mashambulizi ya kuvizia katika vijiji vya mbali. 

Tags