Jan 08, 2022 02:49 UTC
  • Spika wa Bunge, Mawaziri Wakuu wa zamani wa Tunisia kupandishwa kizimbani

Spika wa bunge lililovunjwa la Tunisia na Mawaziri Wakuu wa zamani wa nchi hiyo watafikishwa kizimbani kwa tuhuma za kukiuka sheria za kampeni za kisiasa na kutobainisha vyanzo vya fedha zao wakati wa kampeni za uchaguzi.

Mwendesha mashtaka wa Tunisia alitangaza Jumatano kuwa ameamua kuwafikisha kizimbani watu 19 akiwamo kiongozi wa chama cha  Ennahda Rached Ghannouchi ambaye ni spika wa buunge lililovunjwa pamoja na   waziri mkuu wa zamani Youssef Chahed. Watu hao watafikishwa mahakamani kwa kukiuka sheria za uchaguzi.  Youssef Chahed alikuwa waziri mkuu tokea Agosti 2016 hadi Februari 2020.

Kati ya wanasiasa wengine ambao watafunguliwa mashitaka ni mwenyekiti wa chama cha Qalb Tounes, Nabil Karoui; mkuu wa Chama cha Wafanyakazi, Hamma Hammami, waziri wa ulinzi wa zamani Abdelkarim Zubeidi,  pamoja na mawaziri wakuu wengine wa zamani Elias Fakhfakh, Mahdi Jumaa na Hamadi Jebali. Mwendesha mashtaka anatazamiwa kuwafikisha mahakamani ili wajibu mashtaka ya kukiuka sheria za kampeni za uchaguzi, kutokuwa na uwazi katika fedha walioztumia katika kampeni za uchaguzi na makosa mengine yanayohusu sheria za uchaguzi wa Tunisia.  Mwendesha Mashtaka wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika amesema ameamua kuwafikisha wanasiasa hao kizimbani baada ya ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu kuhusu uchaguzi wa mapema wa rais uliofanyika mwaka 2019.

Ikumbukwe kuwa mnamo Julai 25 mwaka 2021, Tunisia ilikumbwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa baada ya  Rais Kais Saied kutangaza kulisimamisha bunge kwa muda sambamba na kuwaondoa madarakani spika wa bunge na waziri mkuu huku akihodhi mamlaka yote ya nchi. 

Kisingizio cha uamuzi huo wa rais wa Tunisia ni kuwa waziri mkuu alizembea katika kazi na hivyo uchumi wa nchi ulidorora na kwamba hakuchukua hatua za kutosha za kukabiliana na janga la COVID-19.

Rais Kais Saied wa Tunisia

Hatua hiyo iliibua taharuki kubwa ya kisiasa Tunisia na inaweza kutajwa kuwa ni mgogoro mkubwa zaidi wa kisiasa tokea mwaka 2011 wakati wa mapinduzi ya wananachi.

Riccardo Fabiani mtaalamu wa masuala ya Afrika Kaskazini anasema: "Hatua hii imepelekea kuibuka mgogoro mkubwa zaidi wa kisiasa tokea wakati wa mapinduzi ya 2011. Mkondo wa matukio ya Tunisia hauko wazi na hatua ya rais ni sawa na kufanya upasuaji gizani." 

Hatua ya Rais Saied ya kuhodhi peke yake madaraka yote ya nchi iliungwa mkono na baadhi ya Watunisia ambao walikuwa wamechoshwa na migogoro ya kisiasa nchini humo. Hata hivyo kuna idadi kubwa ya watu waliopinga hatua hiyo ambao wanasema nchi hiyo inaelekea katika udikteta na utawala wa kiimla.

Hivi sasa Rais wa Tunisia anatumia Idara ya Mahakama kuwafuta na kuwaadhibu wapinzani wake hasa Rached Ghannouchi kiongozi wa chama cha Ennahda ambacho kimeshadidisha upinzani wake kwa hatua zilizochukuliwa na rais ambamba na kuonya juu ya uwezekano wa kurejea nchi hiyo katika zama za udikteta.

Chama chenye mielekeo ya Kiislamu cha  Ennahda kina ushawishi mkubwa na kimesema kukamatwa mwanachama wake mwandamizi ni uthibitisho wa ukweli wa indhari yake kuhusu kurejea Tunisia katika enzi za udikteta.

Noureddine Bhiri, Naibu Mwenyekiti wa Ennahda  alikamatwa Disemba 31, 2021 kwa tuhuma za ugaidi na kabla ya hapo pia wanasiasa kadhaa walifikishwa katika mahakama ya kijeshi kwa tuhuma za 'kuivunjia heshima Ofisi ya Rais,' hatua ambayo imekosolewa vikali na mashirika ya kutetea haki za binadamu.

Rais wa Tunisia ametangaza kuanza mchakato mashauriano kuhusu katiba mpya na amewataka wananchi wawasilishe maoni yao kuanzia Januari 1 hadi Machi 20, 2021. Hii ni katika hali ambayo bunge limevunjwa na kumeundwa serikali yenye mamlaka dhaifu inayoongozwa na Waziri Mkuu Bi. Najla Bouden-Romadane ambaye aliteuliwa Oktoba 11 2021. Rais Saied aliongeza muda wa kusitishwa kazi za bunge  na kusema kura ya maoni kuhusu katiba itafanyika Julai 25 na uchaguzi wa bunge nao utafanyika Disemba 17, mwaka huu wa 2022.

Kwa muda mrefu Tunisia imekuwa nembo ya mwamko wa wananchi katika nchi za Kiarabu. Lakini sasa baada ya kupita miaka 10 tokea yaibuke mapinduzi ya wananchi, bado nchi hiyo haijaweza kupata utulivu wa kisiasa. Wapinzani wanadai kuwa, hatua ambazo rais anachukua zinairejesha nchi hiyo katika zama za udikteta za wakati wa utawala wa Ben Ali aliyepinduliwa mwaka 2011 kufuatia mwamako wa wananchi uliomlazimisha kukimbia nchi.

Tags