Jan 08, 2022 12:35 UTC
  • Misri yamvua uraia mtetezi wa haki za binadamu

Mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini Misri, Ramy Shaath ameachiwa huru baada ya kuwekwa korokoroni kwa zaidi ya miaka 2 na nusu.

Familia ya mwanaharakati huyo imesema leo Jumamosi kuwa, Shaath ameachiwa huru na vyombo vya usalama vya Misri, kwa sharti la kutakiwa akane uraia wake.

Familia hiyo imesema katika taarifa kuwa, "hakuna anayepaswa kulazimishwa kuchagua ama uraia au uhuru wake." Ramy Shaath ambaye aliachiwa huru Alkhamisi iliyopita, ameelekea Ufaransa anakoishi mke wake.

Ramy ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Nabil Shaath, alikamatwa pamoja na wanaharakati wengine 12 na kuwekwa kizuizini tokea mwaka 2019, kwa tuhuma kuwa walifadhiliwa na harakati ya Ikhwanul Muslimin kwa ajili ya kufanya jinai na kuchochea mapinduzi.

Katika miezi ya karibuni, asasi nyingi za kimataifa na za kutetea haki za binadamu zimetoa indhari kuhusu utendaji wa utawala wa Misri unaoongozwa na Sisi katika masuala ya uhuru wa kijamii na kisiasa na ukiukaji wa haki za binadamu.

 

Rais Sisi anayeiongoza Misri kwa ngumi ya chuma

Baada ya kuongoza mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali halali na ya kidemokrasia ya Muhammad Morsi, Abdul Fattah al-Sisi alishika hatamu za utawala nchini Misri kufuatia uchaguzi wa kimaonyesho wa rais uliofanyika mwaka 2014.

Tangu wakati huo hadi sasa na kwa kutegemea uungaji mkono wa Magharibi, rais huyo wa Misri amekuwa akitekeleza sera ya ukandamizaji dhidi ya wapinzani wa utawala wake.

 

Tags