Jan 11, 2022 14:17 UTC
  • Sheikh Abdillahi Nassir Juma Bhalo
    Sheikh Abdillahi Nassir Juma Bhalo

Sheikh Abdillahi Nassir Juma Bhalo, msomi maarufu wa Kiislamu barani Afrika na hasa Afrika Mashariki ameaga dunia mapema leo Mombasa, Kenya.

Umma wa Kiislamu umetumbikia katika majonzi makubwa kufuatia kuaga dunia Sheikh Abdillahi Nassir, ambaye alitumia umri wake wote uliojaa baraka kuhudumia Uislamu na Waislamu hususan wa kanda ya Mashariki na katikati mwa Afrika

Sheikh Abdillahi Nassir alikuwa mfuasi wa madhehebu ya Ahul Bayt wa Mtume Muhammad SAW na alipata umaarufu kama mwanazuoni, mwalimu, mhadhiri na mwandishi maarufu wa Kiislamu mbali na kuwa miongoni mwa wajumbe wa  Kenya katika mazungumzo ya kupigania uhuru ya Lancaster huko London mwaka 1960

Marehemu alikuwa mwanachuoni mchamungu, mvumilivu, mnyenyekevu na mpambanaji katika njia ya Mwenyezi Mungu na hakuacha kushauri, kutoa miongozo na maelekezo hadi mwisho wa uhai wake.

Sheikh Abdillahi Nassir ameandika vitabu mbalimbali kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza, vilivyosaidia pakubwa kujenga na kukuza imani za Waislamu. Baadhi ya vitabu hivyo vimefasiriwa kwa kadhaa za kigeni.

Katika miaka ya karibuni amekuwa akijishughulisha na uandishi wa tafsiri ya Qur’ani Tukufu kwa lugha ya Kiswahili na kueneza mafundisho ya Ahlul Bayyt (as). Miongoni mwa vitabu vya marehemu Sheikh Abdillahi Nassir ni Shia na Qur'ani, Maulidi si Bidaa, Si Haramu, Ukweli wa Hadithi ya Kisaa, Mut'a Ndoa Halali, Ukweli wa Hadithi ya Karatasi, Ahlul Bayt Ni Nani? na Yazid Hakuwa Amirul Muuminin.

Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran inachukua fursa hii kutuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu Sheikh Abdillahi Nassir, wanafunzi wake, na Waislamu wote kwa ujumla na tunamuomba Mwenyezi Mungu amrehemu na amlipe ujira mwema kwa huduma zake kubwa kwa Uislamu. 

Tags