Jan 14, 2022 08:01 UTC
  • Rais wa Burkina Faso, Sanakara, alipigwa risasi saba

Rais aliyependwa na wananchi wa Burkina Faso, Thomas Sankara, aliuawa kwa kupigwa risasi mara saba, wataalamu wameiambia mahakama wakati wa kusikilizwa kesi ya mauaji ya kiongozi huyo.

Mtaalamu wa masuala ya mwili wa mwanadamu Robert Soudre ameiambia mahakama katika mji mkuu Ouagadougou kuwa Sankara aliuawa kwa kupigwa risasi mara saba kifuani ambapo risasi moja ilifyatuliwa kutoka nyuma.

Rais wa zamani wa Burkina Faso Blaise Compaore na watu wengine 13 wanakabiliwa na mashtaka ya kuhusika na mauaji ya Sankara, ambaye wafuasi wake wanamuita kuwa  ni Che Guevara wa Afrika.

Sankara alikuwa kepteni katika jeshi wakati alipoingia madarakani akiwa na umri wa miaka 33 katika mapinduzi ya 1983.

Alikuwa mashuhuri kutokana na sera zake za kupinga mabeberu na kuwatetea wanyonge. Sankara na wenzake 12 walipigwa risasi Oktoba 15 mwaka 1987 katika kikao cha Baraza la Kitaifa la Mapinduzi.

Taarifa zinabaini kuwa Ufaransa ilihusika na mauaji hayo kutokana na kuwa Sankara alipinga ukoloni mamboleo wa Paris barani Afrika.