Jan 15, 2022 10:41 UTC
  • Maandamano dhidi ya serikali nchini Tunisia katika maadhimisho ya mapinduzi ya Januari 14

Sambamba na kumbukumbu ya mwaka wa 11 wa harakati ya wananchi wa Tunisia iliyopelekea kupinduliwa serikali ya dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Zine El Abidine Ben Ali, Tunisia jana Ijumaa ilishuhidia maandamano makubwa ya kupinga utendaji wa kiongozi wa sasa wa nchji hiyo, Kais Saied.

Maandamano makubwa zaidi yalifanyika kwenye Mtaa wa Habib Bourguiba ambao waandamanaji walipiga nara za kuipinga serikali ya Rais Kais Saied. Maandamano hayo yalizimwa na vikosi vya serikali.

Yamina Zoghlami ambaye ni miongoni mwa viongozi wa vuguvugu la Ennahda nchini Tunisia amesema kuwa, askari usalama walijaa mitaani na kushambulia waandamanaji, waandishi habari na wanasheria. Hapo awali Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia iliwataka wananchi wasikiuke uamuzi maalumu wa Rais wa kuahirisha au kufuta maandamano katika maeneo ya wazi. 

Tunisia ilikumbwa na misukosuko mingi ya kisiasa baada ya harakati ya wananchi ya mwaka 2011 iliyoiondoa madarakani serikali ya rais wa wakati huo, Ben Ali. Nchi hiyo imekuwa ikikabiliwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa, hasa katika miezi ya hivi karibuni baada ya hatua ya Rais Kais Saied kulivunja Bunge na kumuondoa madarakani waziri mkuu. Kisingizio cha uamuzi huo wa Rais wa Tunisia ni kuwa waziri mkuu alizembea katika kazi na hivyo uchumi wa nchi ulidorora na kwamba hakuchukua hatua za kutosha za kukabiliana na janga la COVID-19. 

Kais Saied

Hatua hiyo imepingwa na wananchi na vyama vya siasa vya Tunisia na imeibua taharuki kubwa ya kisiasa na kutajwa kuwa ni mgogoro mkubwa zaidi wa kisiasa tokea mwaka 2011 wakati wa mapinduzi ya wananachi. Spika wa bunge lililosimamishwa la Tunisia, Rached Ghannouchi ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Ennahda amesema, Kais Saied anataka kuhuisha tajiriba iliyofeli na kwamba Tunisia imerejea kwenye kipindi cha udikteta na kutengwa. Muungano wa Wafanyakazi wa Tunisia hivi karibuni pia ulizitaja hatua za rais wa nchi hiyo kuwa ni jaribio la kudhibiti kikamilifu mamlaka ya nchi na umeuonya kwamba Tunisia inaburutwa kwenye shimo la maangamizi. 

Wananchi wengi wa Tunisia wanaamini kwamba hatua za Saied zinapingana na malengo ya vuguvugu la wananchi na kwamba zitarejesha tena udikteta nchini Tunisia. Wengi wao wana wasiwasi kwamba, mustakabali wa nchi hiyo, kwa mara nyingine tena, utaangukia mikononi mwa wale wanaoendeleza njia ya dikteta wa zamani wa nchi hiyo Zine El Abidine Ben Ali. 

Mtaalamu wa siasa wa Tunisia Basil Turjuman anasema: "Tuko mwanzoni mwa awamu mpya ambayo inahitaji mtazamo mpya wa kisiasa, kiuchumi na kijamii ili kuchora mustakabali wa Tunisia, na wala sio kurudi nyuma na kwenye mambo ambayo wananchi wameyavuka."

Alaa kulli hal, hali ya Tunisia imekuwa mbaya zaidi kutokana na kuongezeka kwa mizozo na kutumiwa njia za kijeshi na kiusalama kukabiliana na malalamiko ya wananchi hususan katika siku ya kumbukumbu ya mapinduzi yao. 

Tunisia

Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana spika wa bunge lililovunjwa la Tunisia, Rached Ghannouchi, ameonya kuwa Tunisia inaelekea kwenye udikteta na kusema kwamba, mbinu ya kuyafuta na kuweka pembeni makundi ya kisiasa nchini Tunisia bado inaendelea. 

Inaonekana kuwa wiki zijazo zitaainisha mwelekeo wa hali ya kijamii na kisiasa nchini Tunisia na wala sio hatima ya rais na mipango yake ya kisiasa pekee, bali pia hatima ya demokrasia ya nchi hiyo.

Tags