Jan 15, 2022 11:09 UTC
  • Rais wa Tunisia akosolewa kwa kuandaa bajeti bila kumshirikisha yeyote

Muungano wa Wafanyakazi Tunisia (UGTT) umemkosoa vikali Rais Kais Saied wa nchi hiyo, kwa kutwaa mamlaka yote ya nchi, na kuandaa bajeti ya nchi yeye binafsi pasi na kuzishirikisha taasisi nyingine husika.

Muungano huo ambao ni ndio mkubwa zaidi wa kutetea maslahi ya wafanyakazi nchini humo ulisema jana Ijumaa kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mwaka wa 11 tangu yajiri mapinduzi ya wananchi ya Tunisia kuwa, Rais Saeid ndiye anayefanya maamuzi yote ya kiuchumi na kifedha nchini humo.

UGTT imemkosoa vikali pia Rais huyo, kwa kuwa na misimamo hasi dhidi ya wafanyakazi wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, ikisisitiza kuwa kiongozi huyo hana azma ya kuleta mabadiliko ya kweli nchini humo.

Disemba mwaka uliomalizika 2021, serikali ya Tunis ilitangaza bajeti ya dola bilioni 20 kwa ajili ya mwaka huu 2022, makadirio ya matumizi ya fedha ambayo yana nakisi ya asilimia 6.7 (dola bilioni 3.2).

Maandamano ya wananchi wa Tunisia

Tunisia imekumbwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa tangu Januari 25 mwaka uliopita 2021. Rais Kais Saied wa nchi hiyo alichukua uamuzi wa ghafla na wa kushangaza wa kusitisha shughuli za Bunge na kuwafuta kazi Spika wa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, na kisha kuchukua udhibiti wa masuala yote ya nchi.

Tangu wakati huo,  wananchi wa Tunisia wamekuwa wakimiminika kwenye mitaa ya mji mkuu wa Tunisia, Tunis katika maandamano ya kumtaka rais huyo ajiuzulu. Jana Ijumaa pia, polisi ya Tunisia ilitumia mabomu ya kutoa machozi na maji ya kuwasha kuvunja maandamano ya wananchi dhidi ya Rais Saeid.

Tags