Jan 15, 2022 12:13 UTC
  • Athari za mabadiliko ya tabianchi; kiangazi chaua mifugo 62,000 Tanzania

Kipindi kirefu cha kiangazi kimeua makumi ya maelfu ya mifugo katika wilaya ya Simanjiro mkoani Manyarahuku, kaskazini mwa Tanzania, huku makali ya ukame yakiendelea kushuhudiwa katika pembe mbalimbali za dunia.

Sendeu Laizer, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Wilaya ya Simanjiro amesema hali ya ukame na kiangazi katika eneo hilo ni ya kutia wasiwasi.

Amesema jumla ya mifugo 62,585, wakiwemo ng'ombe 35,746, kondoo 15,136, mbuzi 10,033 na punda 1,670 wamekufa kutokana na makali ya kiangazi kwenye wilaya hiyo.

Naye Christopher Ole Sendeka, Mbunge wa jimbo la Simanjiro amesema kiangazi hicho kimewalazimisha baadhi ya wafugaji kuvuka mpaka na kuingia katika nchi jirani kwa ajili ya kuwalisha mifugo yao.

Kwa mujibu wa takwimu za Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ambao uko chini ya Umoja wa Mataifa, idadi ya watu waliokaribia kukumbwa na janga la ukame imeongezeka kutoka milioni 34 hadi milioni 41 katika pembe mbalimbali za dunia.

Shirika hilo la UN limetangaza kuwa, idadi ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa katika nchi 43 duniani imeongezeka hadi kufikia milioni 45, wakati njaa ikiongezeka kote ulimwenguni.

Tags