Jan 16, 2022 07:54 UTC
  • Jenerali Haftar, mbabe wa kivita wa Libya aitembelea Israel

Mbabe wa kivita na jenerali muasi wa Libya Khalifa Haftar ameripotiwa kufanya safari ya siri ya kuutembelea utawala wa Kizayuni wa Israel, huku duru za habari zikieleza kuwa maafisa wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika wanaandamwa na mashinikizo ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo bandia.

Televisheni ya Russia al-Yaum inayotangaza kwa lugha ya Kiarabu imenukuu vyombo vya habari vya Kiebrania vilivyoripoti kuwa, ndege iliyokuwa imbeba Haftar, siku ya Alkhamisi ilitua katika uwanja wa ndege wa Ben Gurion mjini Tel Aviv, na kuondoka masaa mawili baadaye.

Novemba mwaka jana, gazeti la Al-Akhbar la Lebanon lilifichua kuwa, utawala wa Israel unaunga mkono wagombea wawili wakuu katika uchaguzi wa rais Libya nao ni jenerali muasi Khalifa Haftar na Saiful Islam Gaddafi, mwanae mtawala wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi. 

Kwa mujibu wa gazeti hilo, utawala wa Israel unafadhilisha zaidi Haftar awe rais wa Libya kwa sababu atafanikisha malengo ya utawala huo ya kuwa na satwa kamili katika ukanda wa Bahari ya Medieterrania.

Saddam, mtoto wa kiume wa jenerali muasi Khalifa Haftar aliyemwakilisha baba yake kutembelea utawala wa Kizayuni hivi karibuni

 

Hivi karibuni, Saddam, mwanae Khalifa Haftar, alitembelea Tel Aviv na kukutana na maafisa wa utawala wa Israel na akawahakikishia kuwa baba yake yuko tayari kuanzisha uhusiano na utawala huo haramu.

Hii ni katika hali ambayo, wiki iliyopita, Abdul Hamid Dbeibah, Kaimu Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa ya Libya alikadhibisha madai kuwa amekutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa Israel mjini Amman Jordan, akiwemo David Barnea, Mkuu wa Shirika la Kijasusi la Utawala wa Kizayuni wa Israel (Mossad).

Waziri Mkuu huyo wa Libya sanjari na kusisitiza kuwa msimamo wa nchi hiyo juu ya kadhia ya Palestina uko thabiti na wazi kabisa, alizungumzia madai ya mkutano huo na kusema: Hilo halijafanyika, na wala halitafanyika katika siku zijazo.

Tags