Jan 16, 2022 12:13 UTC
  • Moto  wateketeza Soko la Karume Dar, Rais Samia atoa pole

Moto mkubwa umeteketeza Soko la Karume jijini Dar es Salaam Tanzania na kupelekea karibu mali zote zilizokuwa humo kuteketea mapema leo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango wametoa Pole kwa wafanyabiashara wa soko la Karume ambalo aghalabu ya bidhaa zake zilikuwa ni nguo za mitumba.

Taarifa zinasema hakuna madhara yaliyopatikana kwa wananchi ukiachia mbali hasara ya mali zilizopotea.

Aidha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla amewataka wafanyabiasha wa soko la Karume lililoungua kuwa watulivu huku akiahidi kuunda kamati itakayochunguza chanzo cha moto huo.

"Chanzo cha moto huo katika soko la Karume au mchikichini bado hakijulikana huku kukiwa na makisio ya hitilafu ya umeme, soko hilo limeungua kwa takribani asilimia 98 licha ya jitihada za kuudhibiti," Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam ameeleza.

Moto ukiteketeza Soko la Karume, Dar es Salaam

Imeelezwa kuwa moto huo ulioteketeza sehemu kubwa ya soko hilo lenye wafanyabiashara zaidi ya 3,500 ulianza usiku wa kuamkia leo huku Jeshi la zimamoto na uokoaji likijitahidi kuuzima lakini ukawa umeteketeza sehemu kubwa ya soko hilo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala amefikisha salamu hizo kwa wafanyabiashara wa soko hilo na kusema kuwa viongozi wa nchi wanawasihi wawe na uvumilivu na kutopeana maneno ya uongo wakisubiri uchunguzi kukamilika.

Amesema kuanzia mida ya saa 9 usiku wahusika wa uzimaji wa moto walijitahidi kudhibiti moto ili usienee katika makazi ya wananchi na kutokana na miundombinu ya soko hilo ugumu ulionekana ingawa kazi kubwa imefanyika.

Itakumbukwa kuwa Julai mwaka jana, Soko la Kariakoo liliungua huku chanzo cha Moto kikiwa hakijafahamika.

Tathmini zilionesha kuwa maduka zaidi ya 220 yalitekeketea kwa moto katika soko la Kariakoo lililopo jijini Dar es salaam.