Jan 17, 2022 02:40 UTC
  • Msemaji wa serikali ya Somalia anusurika kuuawa, ajeruhiwa katika mlipuko Mogadishu

Msemaji wa serikali ya Somalia jana Jumapili alijeruhiwa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Mogadishu katika shambulio la kigaidi la kujilipua kwa bomu.

Mpiga picha mmoja aliyekuwepo eneo la tukio ameripoti kuwa, vipande vya mwili vilikuwa vimetapakaa ardhini nje ya nyumba ya Mohamed Ibrahim Moalimuu msemaji wa serikali ya Somalia ambaye amenusurika kuuliwa hiyo jana. Baada ya tukio hilo, msemaji wa serikali ya Somalia  alikimbizwa hospitali kwa matibabu.

Mohamed Ibrahim Moalimuu

Shirika la habari la Somalia limetangaza kuwa, mlipuko huo uliotokea katika makutano ya barabara mjini Mogadishu ulitekelezwa na mtu aliyekuwa amejifunga bomu. Akiripoti kutoka Mogadishu, Jamae Nour mwandishi wa televisheni ya al Jazeera ameeleza kuwa hii si mara ya kwanza kwa Moalimuu, mwandishi habari wa zamani, kuokoka jaribio la mauaji. 

Wapiganaji wa kundi la wanamgambo wa al Shabab na mtandao wa al Qaida wanayotekeleza hujuma mbalimbali kwa shabaha ya kuing'oa madarakani serikali ya Somalia inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, wamekuwa wakidai kuhusika na mashambulio mbalimbali huko Somalia na nje ya nchi hiyo. 

Ilitarajiwa pakubwa kwamba, machafuko yataongezeka huko Somalia kufuatia kuakhirishwa uchaguzi mkuu kwa karibu mwaka mmoja sasa. 

Tags