Jan 17, 2022 12:22 UTC
  • Tume ya Uchaguzi Kenya yaanza awamu ya pili ya uandikishaji wapiga kura

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC) imeanza awamu ya pili ya kuwasajili wapiga kura kote nchini humo ikiwa ni maandalizi ya kuelekea uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.

Tume hiyo iliyoshindwa kutimiza malengo ya kuandikisha wapiga kura milioni sita kwenye awamu ya kwanza iliyofanya mwaka uliopita katika awamu hii ya pili inalenga kuandikisha wapiga kura milioni 4.5 wakati huu, zoezi hilo litakapokamilika tarehe sita Februari mwaka huu.

Ili kufikia malengo yake kwenye zoezi hili, Tume ya IEBC imeambaza vifaa vya kuwasajili wapiga kura katika wadi zote kote nchini humo, huku ikilenga kuhakikisha kuwa wapiga kura milioni 25 wanashiriki katika upigaji kura, tarehe tisa Agosti mwaka huu.

Tume hiyo ilianza zoezi la kuwaandikisha wapiga kura tarehe nne Oktoba hadi tarehe tano Novemba mwaka uliopita ambapo wapiga kura wapya milioni 1.5 waliandikishwa.

Wafula Chebukati, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC)

 

Wafula Chebukati, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC) amesema kuwa wataruhusu wapiga kura wanaotaka kubadilisha vituo vya upigaji kura.

Wapiga kura walioko nje ya nchi ya Kenya wataanza kuandikishwa tarehe 21 hadi tarehe sita mwezi Februari, zoezi hilo litakapokamilika. IEBC inalenga kuandikisha wapiga kura katika mataifa ya Uingereza, Marekani, Sudan Kusini, Qatar, Umoja wa Falme za Kiarabu na Ujerumani.

Punde tu baada ya zoezi la kujiandikisha litakapokamilika, ukaguzi wa sajili ya wapiga kura itafanyika kisha walioandikishwa kuthibitishwa.

Ukosefu wa vitambulisho ulisemekana kuchangia uandikishaji mdogo mwaka uliopita. Hata hivyo vijana wametoa sababu tofauti za kutojiandikisha kwa wingi.