Jan 17, 2022 15:03 UTC
  • Tanzania na Burundi zatiliana saini mkataba wa zaidi ya dola milioni 900 wa njia ya reli

Nchi mbili za Tanzania na Burundi zimetiliana saini makubaliano ya ujenzi wa njia ya reli itakayogharimu zaidi ya dola milioni 900 za Kimarekani kwa ajili ya kuimarisha biashara baina ya nchi hizo mbili jirani. Makubaliano hayo yametiwa saini mkoani Kigoma, mkoa wa magharibi mwa Tanzania unaopakana na Burundi.

Njia hiyo ya reli itakuwa na urefu wa kilomita 282 na itaiunganisha Burundi na Tanzania kutokea mji mkuu wa kiserikali wa Burundi yaani Gitega na mji wa Uvinza mkoani Kigoma kwa upande wa Tanzania.

Waziri wa Fedha wa Tanzania Mwigulu Nchemba amesema kuwa, nchi hizo mbili zitagharamia mradi huo ambao gharama yake haitopindukia dola milioni 950 za Kimarekani.

Kwa upande wake, Capt Diedonne Dukundane, Katibu Mtendaji wa Central Corridor wa Burundi amesema wakati wa utiaji saini mkataba huo kama ninavyomnukuu: "Ni mradi muhimu sana kwa sababu ukiangalia mzigo unaokusudiwa kusafirishwa kutoka Msongati pale Burundi ni mzigo wa zaidi ya tani milioni moja na 50. Na ukijumlisha na madini mengine yanayopatikana katika eneo la Nemkere pale karibu na Msongati ni zaidi ya tani milioni tatu, huo mzigo ni mkubwa utachimbwa na utasafirishwa zaidi ya miaka 50" 

Picha ya pamoja baada ya kutiwa saini mkataba wa ujenzi wa njia ya reli baina ya Tanzania na Burundi

 

Naye Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Tanzania amesema kama ninavyomnukuu: "Mradi huu ni muhimu sana, kwanza utafungua njia kwa upande wa Burundi na Tanzania; kama mnavyojua Burundi na DRC nchi hizo zote zinategemea bandari ya Dar es Salaam kwa kupeleka mizigo yao na kupokea mizigo yao, sasa kufunguka kwa kupitia njia ya reli, hiyo itasaidia sana.  

Tanzania ni lango muhimu la kuingiza na kusafirisha bidhaa kwa nchi zisizo na bahari kama Burundi, Rwanda, Uganda, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.