Jan 17, 2022 15:10 UTC

Wafanya biashara wa soko la mitumba la Mchikichini wilayani Ilala jijini Dar es Salaam Tanzania wameandamana na kufunga barabara kuishinikiza serikali iwaruhusu waendelee na biashara zao licha ya soko hilo kuunga usiku wa kuamkia jana Jumapili. Baada ya maandamano hayo, serikali imewaruhusu waweke alama kwenye maeneo yao wakati wakisubiri ripoti ya kamati ya kuchunguza chanzo cha moto ya jana.

Toleo la mtandao la gazeti la kila siku la Mwananchi limeripoti habari hiyo na kusema kuwa, polisi mkoani Dar es Salaam wametumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafanyabiashara wa soko hilo la Karume (Mchikichini) ambao wameandamana na kufunga barabara iliyopo karibu na ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Amos Makalla wakishinikiza kuruhusiwa kuendelea na biashara katika soko hilo.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, wafanyabiashara hao maarufu machinga wamefunga barabara kwa kutumia mawe na magogo katika makutano ya barabara ya Uhuru na Kawawa Ilala Boma muda mfupi baada ya kuandamana mpaka kwenye geti la  Ofisi ya Mkuu huyo wa Mkoa huku wakidai kuwa wanataka Amos Makalla awaruhusu waendelee kufanya shughuli zao kwenye soko hilo.

Waandamanaji jijini Dar es Salaam Tanzania wakitaka waruhusiwe kuendelea na biashara katika soko lolilounga la mitumba la eneo la Karume, wilayani Ilala

 

Mkanda wa video uliorushwa na toleo la mtandao la gazeti hilo unawaonesha wafanya biashara hao wakisema kwa hamasa kubwa "Tunataka Soko Letu" huko moja ya mabango ya waandamanaji hao likiwa na maandishi yanayosema: "Serikali sikivu husikiliza wananchi wake."

Ripoti hiyo imeongeza kuwa, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng'wilabuzu Ludigija aliwaomba wafanyabishara hao kuwa wavumilivu na kufuata utaratibu uliotangazwa na Serikali kwamba waiachie kamati ifanye kazi kwa siku saba na kutoa ripoti badala ya kuandamana kutaka kushindana na Serikali.

Jana Jumapili baada ya soko hilo kuungua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla aliwataka wafanyabiasha wa soko hilo kuwa watulivu na kuahidi kuunda kamati ambayo itachunguza chanzo cha moto huo kwa siku 14 akipiga marufuku shughuli zozote kuendelea wakati wa uchunguzi huo.