Jan 18, 2022 13:17 UTC
  • Zaidi ya dola milioni 138 zahitajika kuwaokoa watu milioni 1.5 Pembe ya Afrika

Zaidi ya dola milioni 138 za ufadhili wa dharura zinahitajika kusaidia watu milioni moja na nusu ambao wako hatarini katika jamii za vijijini kwenye ukanda wa Pembe ya Afrika. Watu hao ni wale ambao mashamba yao na malisho ya mifugo yameathiriwa na ukame wa muda mrefu.

Hayo yamesemwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO mjini Roma nchini Italia wakati lilipokuwa linatoa ripoti ya kina kuhusu mpango wa kukabiliana na changamoto za kilimo na aina ya msaada unaoitajika kwa kila kanda.

Pembe ya Afrika ni eneo ambalo tayari linakabiliwa na uhaba wa chakula unaotokana na hali mbaya ya hewa, vikwazo vya maliasili na migogoro, janga la UVIKO-19 na uvamizi wa nzige uliotokea 2020-2021 ambao umefanya jamii za ukanda huo kukabiliana na changamoto nzito hadi kufikia kudhoofisha vibaya mazao ya kilimo.

Ukame umesababisha matatizo makubwa katika eneo la Pembe ya Afrika

 

Kwa mujibu wa FAO, nchi za Ethiopia, Kenya na Somalia, ndizo zilizoathirika zaidi. Makadirio yanaonesha kuwa, takriban watu milioni 25 na laki 3 watakuwa hawana uhakika wa chakula ifikapo katikati ya mwaka wa 2022.

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa, iwapo misaada ya dharura haitopatikana na hali hiyo itatendelea basi nchi za ukanda wa Pembe ya Afrika zitakuwa kati ya nchi zinazokabiliwa na mgogoro mkubwa wa chakula duniani.

Si hayo tu, lakini pia kwa mujibu wa Shirika la Uhamiaji la Kimataifa IOM,  janga la corona limeongeza hatari kwa wahamiaji kutoka Pembe ya Afrika ya kuuzwa kimagendo, kuzidi kuwa maskini kutokana na mabadiliko ya ghafla ya hali ya hewa na kukosa huduma za msingi.