Jan 18, 2022 13:39 UTC
  • Watu 12,000 wanashikiliwa rasmi kororokoni Libya, maelfu wanashikiliwa kinyume cha sheria

Umoja wa Mataifa umetoa ripoti maalumu ya uvunjaji wa haki za binadamu na kusema kuwa, nchini Libya kuna watu 12,000 wanashikiliwa rasmi korokoroni na maelfu ya wengine wanashikiliwa kinyume cha sheria na bila ya kutangazwa.

Umoja huo umesema, kwa mujibu wa takwimu rasmi, kuna watu 12 elfu na 27 wanaoshikiliwa nchini Libya lakini pia kuna maelfu ya watu wengine wanashikiliwa nchini humo kinyume cha sheria. Wengi wa watu hao wanaishi katika mazingira mabaya na magumu mno ya kibinadamu, wanadhibitiwa na magenge yenye silaha na taasisi za siri.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa, timu ya wanasiasa wa umoja huo iliyotumwa huko Libya imesema kuwa hadi hivi sasa bado kunashuhudiwa kesi nyingi za kutiwa watu mbaroni kiholela, kuteswa na matukio mengine ya uvunjaji wa haki za binadamu katika majengo yanayodhibitiwa na serikali na makundi mengine nchini humo.

Wakimbizi nchini Libya

 

Hayo yameripotiwa huku watu wanaokamatwa na kuwekwa korokoroni wakiwa hawana uwezo wa kujitetea wala kulalamikia kushikiliwa kwao kinyume cha sheria.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres amesema kuhusu ripoti hiyo kwamba, bado ana wasiwasi mkubwa wa kuendelea uvunjaji wa mara kwa mara na wa daima wa haki za binadamu hasa dhidi ya wahajiri, wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi nchini Libya.

Huku hayo yakiripotiwa, Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya Bi Stephanie Williams amesema kuwa, kipaumbeke kikuu zaidi hivi sasa kuhusu Libya ni kuweko maridhiano ya kitaifa na kusisitiza kuwa wananchi wa Libya hawataki tena vita na kuna haja ya kuchukuliwa hatua za dhati za kufanikisha mapatano ya kitaifa nchini humo.