Jan 20, 2022 04:25 UTC
  • Watu 220 wameuawa Nigeria tangu mwaka huu uanze

Kwa akali watu 220 wameuawa katika mashambulio ya magenge ya kigaidi na makundi ya uhalifu na ujambazi katika jimbo la Niger nchini Nigeria.

Hayo yamesemwa na Gavana wa jimbo hilo, Abubakar Sani Bello, katika kikao na waandishi wa habari baada ya kufanya mazungumzo na Rais Muhammadu Buhari katika Ikulu ya Abuja.

Gavana Bello amesema mashambulio zaidi ya 50 yameshuhudiwa katika jimbo hilo la katikati mwa nchi, katika kipindi cha kuanzia Januari Mosi hadi Januari 17.

Kadhalika amesema watu wasiopungua 200 wakiwemo raia watatu wa China wametekwa nyara katika jimbo hilo katika muda huo wa chini ya wiki tatu.

Mauaji yanaendelea licha ya vikosi vya ulinzi Nigeria kufanya operesheni za kuyatokomeza magenge ya ugaidi na uhalifu

Gavana wa jimbo la Niger ameongeza kuwa, wabeba bunduki waliotekeleza mauaji hayo wanaendesha pia operesheni kama hizo za kushambulia vijiji na kutekeleza mauaji katika majimbo yanayopakana na jimbo hilo, ambalo ndilo kubwa zaidi katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Haya yanajiri huku maeneo ya kaskazini na kaskazini mashariki mwa Nigeria yakiendelea kushuhudia ongezeko kubwa la vitendo vya uhalifu huku serikali ya Buhari ikiwa mbioni kurejesha amani bila mafanikio. 

Tags