Jan 21, 2022 03:16 UTC
  • Mali yataka mkataba wa ushirikiano wake wa kijeshi na kiulinzi na Ufaransa upitiwe upya

Serikali ya Mali inapanga kupitia upya mkataba wa ushirikiano wa kijeshi na kiulinzi kati yake na Ufaransa. Mkataba huo kati ya nchi hizo mbili ulitiwa saini mwaka 2014 na kuanzisha operesheni Barkhane ili kuisaidia Mali kupambana na makundi ya kigaidi.

Mnamo mwezi uliopita wa Desemba Paris na Bamako zilikuwa zimekubaliana kuongeza muda wa mkataba huo kwa miaka mitano zaidi.

Miongoni mwa masuala yaliyomo katika mkataba huo ni namna ya kuwalinda wanajeshi wa Ufaransa; na uhuru wao wa kutembea katika maeneo ya Mali waliko askari wenzao wa Kifaransa.

Hata hivyo Mali sasa imeonekana kutaka mkataba huo upitiwe upya, baada ya kuishutumu Ufaransa kuvunja utaratibu, kwa kupaa ndege yake ya kivita katika anga ya nchi hiyo.

Licha ya kuunga mkono vikwazo vya kiuchumi iliyowekewa Mali na nchi za Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, Ufaransa imesema itaendelea kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Mali na kusaidia katika mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi ya DAESH (ISIS) na Al Qaeda.

Nchi ya Mali imekuwa ikisumbuliwa na uasi na machafuko ya ndani tangu mwaka 2012. 

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa, MINUSMA na wanajeshi wa Ufaransa walitumwa huko Mali katikati ya mwaka 2013 kwa shabaha ya kurejesha amani na utulivu nchini humo, lakini majeshi hayo hayakuwa na mafanikio ya kuridhisha; na nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika ingali inasumbuliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya makundi ya kigaidi.../ 

 

 

 

Tags