Jan 21, 2022 08:00 UTC
  • 17 wapoteza maisha 59 wajeruhiwa katika mripuko mkubwa wa lori nchini Ghana

Watu wasiopungua 17 wameripotiwa kufa na wengine 59 wamejeruhiwa katika mripuko mkubwa uliotokea usiku wa kuamkia leo Ijumaa magharibi mwa Ghana baada ya lori lililokuwa limebeba mada za miripuko kugongana na piki piki na kuripuka.

Mripuko huo umechimba shimo kubwa na kuharibu mamia ya nyumba karibu na mji wa Bogoso ulioko umbali wa takriban kilomita 300 kutoka mji mkuu Accra. Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa, watu wameonekana wakikimbilia kwenye eneo la tukio hilo huku moto mkubwa pamoja na moshi mzito ukionekana ukipanda angani. 

Duru rasmi za serikali ya Ghana zimesema kuwa, nyumba zisizopungua 500 zimeharibiwa na mripuko huo mkubwa. Hadi wakati inaripotiwa habari hiyo, watu wasiopungua 17 walikuwa wamethibitishwa kufa na wengine 59 wamejeruhiwa. Hayo ni kwa mujibu wa Waziri wa Habari wa Ghana, Kojo Oppong Nkurumah alipotoa taarifa rasmi jana usiku. 

Kijiji cha Apiate cha karibu na mji wa Bogoso kimeathiriwa vibaya na mripuko huo

 

Waziri Nkurumah amesema, taarifa za awali zinaonesha kuwa ajali hiyo imetokea baada ya lori lililokuwa na miripuko kugongana na pikipiki na gari nyingine iliyokuwa inapita karibu na transfomer ya umeme. Amesema, kati ya majeruhi hao 59, 42 wanaendelea na matibabu mahospitalini huku baadhi yao wakiwa na hali mbaya.

Serikali ya Ghana imeitaka miji mingine ya nchi hiyo kutenga maeneo ya umma kama vile mashule na viwanja vya michezo kwa ajili ya kuwahifadhi wahanga na waathiriwa wa mripuko huo. Rais Nana Akufo-Addowa wa Ghana amesema, ajali hiyo ni ya kusikitisha sana, ni janga kubwa na ametoa mkono wake wa pole kwa familia za wahanga na waathiriwa wote wa tukio hilo.