Jan 23, 2022 07:56 UTC
  • AU yaunga mkono kipindi cha mpito cha miezi 16 nchini Mali

Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limetangaza kuwa umoja huo unaunga mkono mamlaka ya serikali ya mpito ya Mali kuongezwa kwa muda mfupi usiozidi miezi kumi na sita.

Baraza la Amani na Usalama la AU lilikutana wiki moja tu iliyopita, lakini mahitimisho ya mazungumzo yake hayakutangazwa hadi Ijumaa ya tarehe 21 Januari. Wakati wa mkutano huu maalumu wa kujadili kadhia ya Mali, baraza hilo liliidhinisha misimamo ya Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS na kuunga mkono vikwazo vilivyowekwa na jumuiya hiyo dhidi ya nchi hiyo.

Taarifa ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika imebainisha chini ya anuani: "Ongezeko lisilofaa la mchakato wa mpito nchini Mali", kwamba, kwa upande wa Umoja wa Afrika, unaona kuwa ratiba iliyopendekezwa na mamlaka ya Mali ya kuongezwa kipindi cha mpito kwa miaka mitano, kisha miaka minne, inachukuliwa kuwa "kinyume cha katiba, hairuhusiwi na haifai na ni kizuizi kikubwa kwa mchakato wa demokrasia nchini humo."

Aidha, taarifa hiyo ya AU imebainisha kuwa, umoja huo unaomba kurejea "haraka" kwa utaratibu wa kikatiba na kidemokrasia "unaoongozwa na raia" na unaunga mkono pendekezo la upatanishi lililotolewa na Algeria na kwamba tarehe ya mwisho iliyopendekezwa na Algiers, isiyozidi miezi kumi na sita ya ziada ya mpito kabla ya kuandaa uchaguzi wa urais na wa wabunge, inachukuliwa kuwa "inafaa na inaweza kufikiwa. 

Sambamba na hayo, taarifa ya Baraza la Amani na Usalama la AU imelaani pia kile ilichosema "kuendelea kufungwa" kwa viongozi wa kisiasa na viongozi wa zamani wa Mali "na mamlaka ya mpito", ambako ni "kinyume cha sheria", na kusisitiza kuwa inapasa watu hao waachiwe.../