Jan 23, 2022 12:19 UTC
  • Milio ya risasi yasikika katika kambi mbili za jeshi katika mji mkuu wa Burkina Faso

Milio mingi ya risasi imekuwa ikisikia tangu mapema leo asubuhi katika kambi ya Jenerali Baba Sy na kambi ya Sangoulé Lamizana katika mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou.

Ripoti zaidi zinasema kwa, hali kama hiyo pia inaripotiwa huko Kaya na Ouahigouya kaskazini mwa nchi.

Sababu na chanzo cha milio hiyo ya risasi hadi tunaingia mitamboni kilikuwa hakijajulikana. Serikali imesema katika taarifa kwa vyombo vya habari, kwamba milio ya risasi "imesikika" katika kambi kadhaa nchini humo lakini imekanusha kuwepo kwa "jaribio la mapinduzi".

Baadhi ya mashuuhuda wameziambia duru za habari kwamba, mara ya kwanza kulisikika risasi za hapa na pale na baada ya muda mchache hali ikawa mbaya zaidi. Huko Kaya, milio ya risasi pia ilisikika katika kambi ya kikosi cha jeshi, na huko Ouahigouya, wakaazi pia wameripoti kuwepo na ufyatuaji risasi katika kambi ya jeshi.

Wanajeshi wa Burkina Faso wakiwa katika doria

Jumamosi ya jana wanajeshi wasiopungua wawili waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mlipuko wa bomu lililotengenezwa kienyeji, kwenye barabara kati ya Ouahigouya na Titao (Kaskazini), wakati gari lao lililokuwa likiwasindikiza wafanyabiashara lilipokanyaga bomu hilo.

Katika miaka ya hivi karibuni Burkina Faso imekuwa shabaha ya mashambulizi mengi ya makundi ya kigaidi yaliyoanzia kaskazini mwa nchi na kisha kuenea mashariki na katikati mwa Burkina Faso. Mwishoni mwa mwaka jana watu wasiopungua 44 waliuawa katika mashambulizi mawili ya kigaidi huko magharbi mwa Burkina Faso.