Jan 24, 2022 02:42 UTC
  • Kambi ya jeshi la Ufaransa nchini Mali yashambuliwa, kadhaa wauawa, kujeruhiwa

Kwa akali askari mmoja wa Ufaransa ameuawa huku wengine kadhaa wakijeruhuwa katika shambulio la roketi dhidi ya kambi ya kijeshi ya nchi hiyo ya Ulaya huko kaskazini mwa Mali.

Wizara ya Ulinzi ya Ufaransa jana Jumapili ilithibitisha habari za kuuawa Brigedia Alexandre Martin wa Kikosi cha 54 cha Jeshi la Ufaransa katika mji wa Gao, kaskazini mwa Mali katika shambulio hilo la roketi.

Aidha taarifa ya wizara hiyo imesema wanajeshi wengine tisa wa Ufaransa wamejeruhiwa katika hujuma hiyo ya Jumamosi jioni. Kwa mujibu wa wizara hiyo, askari 54 wa Ufaransa wameuawa kufikia sasa katika hujuma za namna hii, tokea mwaka 2014.

Maandamano ya Wamali ya kutaka kuondoka nchini humo wanajeshi wa Ufaransa

Haya yanajiri wakati huu ambapo, serikali ya Mali inapanga kupitia upya mkataba wa ushirikiano wa kijeshi na kiulinzi kati yake na Ufaransa. Mkataba huo kati ya nchi hizo mbili ulitiwa saini mwaka 2014 na kuanzisha Operesheni ya Barkhane ili kuisaidia Mali kupambana na makundi ya kigaidi.

Nchi ya Mali imekuwa ikisumbuliwa na uasi na machafuko ya ndani tangu mwaka 2012, licha ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa (MINUSMA) na wanajeshi wa Ufaransa kutumwa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi tokea mwaka 2013, kwa shabaha ya kurejesha amani na utulivu nchini humo

Tags