Jan 24, 2022 09:50 UTC
  • Rais wa Burkina Faso, Christian Kabore, azuiliwa katika kambi ya kijeshi

Rais wa Burkina Faso, Roch Kabore, anazuiliwa na wanajeshi waasi katika kambi ya kijeshi. Hayo yamesemwa leo na vyanzo viwili vya usalama na mwanadiplomasia wa Afrika Magharibi kufuatia milio ya risasi iliyosikikka kandokando ya makazi ya kiongozi huyo Jumapili usiku katika mji mkuu, Ouagadougou.

Jumapili ya jana serikali ya Burkina Faso ilikanusha uvumi kwamba kumefanyika mapinduzi ya kijeshi huku milio ya risasi ikiendelea kusikika kwa saa kadhaa katika baadhi ya kambi za jeshi. 

Msemaji wa serikali amesema kwamba mazungumzo yanaendelea na wanajeshi hao waasi.

Hali ya mchafukoge imeongezeka katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi katika miezi ya hivi karibuni kutokana na mauaji ya mara kwa mara ya raia na wanajeshi yanayofanywa na wanamgambo ambao baadhi yao wana mfungamano na makundi ya kigaidi ya Daesh na al Qaida.

Jana Jumapili wananchi walijitokeza kuwaunga mkono waasi na kuvamia makao makuu ya chama cha kisiasa cha Rais Kabore. Hiyo jana pia Serikali ya Burkina Faso ilitangaza amri ya kutotoka nje nyakati za usiku hadi alfajiri ya leo na imefunga shule kwa siku mbili.

Wananchi wakiwaunga mkono wanajeshi waasi, Burkina Faso

Katika miaka ya hivi karibuni Burkina Faso imekuwa shabaha ya mashambulizi mengi ya makundi ya kigaidi yaliyoanzia kaskazini mwa nchi na kisha kuenea mashariki na katikati mwa Burkina Faso. Mwishoni mwa mwaka jana watu wasiopungua 44 waliuawa katika mashambulizi mawili ya kigaidi huko magharbi mwa Burkina Faso.