Jan 24, 2022 14:03 UTC
  • Maelfu waendeleza maandamano ya kupinga utawala wa kijeshi nchini Sudan

Maelfu ya wananchi wa Sudan leo Jumatatu wameendeleza maandamano ya kupinga utawala wa kijeshi na kutaka majenerali wa kijeshi warudi makambini na waachie wananchi waendeshe utawala wa kiraia nchini humo.

Maandamano ya nchini Sudan yanaendelea kwa miezi kadhaa sasa tanga wanajeshi walipofanya mapinduzi mengine mwishoni mwa mwezi Oktoba 2021 ambayo yaliiondoa madarakani serikali iliyokuwa inashirikisha raia nchini humo. 

Waandamanaji wameendeleza maandamano katika miji mikubwa ya Sudan ukiwemo wa Wad Madani wa kusini mwa mji mkuu wa Khartoum ambao ni makao makuu ya jimbo la Gedaref. Waandamanaji wamepaza sauti zao wakisema: "Hapana, hatutaki utawala wa kijeshi" na "utawala wa raia ndilo chaguo la wananchi."

Maandamano yamekuwa ni suala la kila siku nchini Sudan tangu tarehe 25 Oktoba mwaka jana wakati majenerali wa kijeshi wakiongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan walipotwaa kwa nguvu madaraka na kuipindua serikali iliyokuwa inashirikisha pia raia.

Jenerali Abdul Fattah al Burhan anayependa kufanya mapinduzi ya kijeshi nchini Sudan

 

Takwimu za madaktari zinasema kuwa, watu 73 wamethibitishwa kuuawa hadi hivi sasa na mamia ya wengine wameshajeruhiwa katika maandamano hayo ambayo licha ya utawala wa kijeshi kuweka sheria kali na kufanya ukandamizaji mkubwa na umwagaji wa damu, lakini wameshindwa kuzuia wananchi kuandamana. 

Siku ya Ijumaa pia maelfu ya wananchi wa Sudan walifanya maandamano makubwa waliyoyapa jina la maandamano ya "Ijumaa ya Shahidi" katika mji wa Khartoum na miji mingine muhimu ya nchi hiyo.

Maandamano hayo ya "Ijumaa ya Shahidi" yaliitishwa na Jumuiya ya Wafanyakazi na asasi nyingine za kiraia kwa ajili ya kuwashinikiza wanajeshi wa nchi hiyo waachie ngazi na kuruhusu demokrasia ichukue mkondo wake.