Jan 25, 2022 02:38 UTC
  • Waziri Mkuu wa Libya ataka katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu

Waziri Mkuu wa Serikali ya Mpito nchini Libya Abdulhamid Dbeibah ametoa mwito wa kupatikana katiba kabla ya uchaguzi wa rais na bunge ulioakhirishwa nchini humo.

Dbeibah amesema katiba inahitajika hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote ili kuilinda nchi na raia wa Libya pamoja na kusimamia chaguzi.  

Katika mjadala uliofanyika mjini Tripoli uliowashirikisha maafisa mbalimbali akiwemo mkuu wa baraza la juu ya serikali, Khaled al Michri, Waziri Mkuu Dbeiba aliongeza kusema kwamba, Walibya wanahitaji uchaguzi huru utakaoheshimu matakwa yao na sio kutanuliwa kwa mgogoro kwa kuwekwa serikali nyingine ya mpito.

Kwa mujibu wa waziri mkuu huyo tatizo kubwa la Linya hivi sasa ni kukosekana katiba.

Uchaguzi wa Libya ulikuwa umepangwa kufanyika tarehe 24 Disemba, mwaka jana 2021 lakini uliakhirishwa kutokana na hitilafu mbalimbali kama za nani wanafaa kugombea na vile vile kutowasilishwa orodha kamili za wagombea.

Usalama umezorota nchini Libya kutokana na kuweko makundi ya wanamgambo na mamluki

 

Tume ya uchaguzi ya Libya imependekeza uchaguzi wa bunge ufanyike mwezi Februari 2022 baada ya kufanyika maandamano mbele ya jengo la tume hiyo ya watu wanaolalamika kwamba hivi sasa mazingira mazuri hayajaandaliwa ya kufanyika uchaguzi kama huo.

Libya ilitumbukia katika machafuko baada harakati iliyoungwa mkono na NATO kumuondoa madarakani mtawala wa muda mrefu wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi mnamo 2011. Machafuko hayo yaliigawa nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta kati ya sehemu mbili za serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataiifa katika mji mkuu, Tripoli, na mamlaka hasimu iliyokuwa uikitawala mashariki mwa nchi hiyo.