Jan 25, 2022 03:32 UTC
  • Jeshi la Burkina Faso lamuengua madarakani Rais Kabore, AU yatoa kauli

Jeshi la Burkina Faso limetangaza kuwa limemuondoa madarakani Rais wa nchi hiyo Roch Marc Christian Kabore, sambamba na kuvunja Bunge na serikali.

Taarifa iliyosainiwa na Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba na kusomwa katika radio na televisheni ya taifa jana Jumatatu na Kapteni Sidsore Kader Ouedraogo, msemaji wa serikali ya kijeshi iliyotwaa mamlaka imeeleza kuwa, jeshi la nchi hiyo limesimamisha pia Katiba.

Taarifa hiyo imesema mapinduzi hayo ya kijeshi yamefanyika pasi na umwagikaji wa damu, na kwamba (maafisa wa serikali) wanaozuiliwa wapo katika sehemu salama.

Jeshi la Burkina Faso ambalo pia limefunga mipaka ya nchi, limesema sababu ya kumuuzulu Rais Kabore ni kutokana na kushtadi ukosefu wa usalama, na kushindwa kiongozi huyo kuliunganisha taifa na kupatia ufumbuzi changamoto zinazolikabili.

Haya yanajiri huku Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) akilaani vikali kile alichokitaja kuwa 'jaribio la mapinduzi ya kjeshi' na kushikiliwa Rais Roch Kabore ambaye alichaguliwa na wananchi kwa njia ya kidemokrasia.

Hali ya mchafukoge nchini Burkina Faso

Moussa Faki Mahamat amewataka wanajeshi wafanya mapinduzi kuhakikisha kuwa rais na mawaziri wanaozuiliwa wapo salama; akisisitiza kuwa mzozo uliopo unapaswa kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo.

Hii ni katika hali ambayo, juzi Jumapili serikali ya Burkina Faso ilikanusha uvumi kwamba kumefanyika mapinduzi ya kijeshi huku milio ya risasi ikisikika kwa saa kadhaa katika baadhi ya kambi za jeshi, na kandokando ya makazi ya kiongozi huyo. Kadhalika siku hiyo ya Jumapili wananchi walijitokeza kuwaunga mkono wanajeshi waasi na kuvamia makao makuu ya chama cha kisiasa cha Rais Kabore. 

Tags