Jan 25, 2022 07:41 UTC
  • Mali yataka Denmark iondoe wanajeshi wake nchini humo

Mali imeitaka Denmark iondoe wanajeshi wake mara moja katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi, ambao walitumwa nchini humo kama sehemu ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Ufaransa.

Katika taarifa, serikali ya Mali imesema imeshangazwa na kitendo cha kutumwa vikosi maalumu vya Denmark nchini humo, kama sehemu ya muungano wa kijeshi wa Ufaransa, ulioko nchini humo 'kupambana na magenge ya ugaidi.'

Taarifa hiyo imefafanua kuwa, Denmark imetuma askari wake nchini Mali pasi na kuishauri au kuitaarifu serikali ya Bamako, na vile vile hatua hiyo imekiuka Protokali ya Ziada inayozihusu nchi za Ulaya washirika wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Haya yameripotiwa wakati huu ambapo serikali ya Mali pia inapanga kupitia upya mkataba wa ushirikiano wa kijeshi na kiulinzi kati yake na Ufaransa.

Askari wa Italia nchini Mali

Mkataba huo kati ya nchi hizo mbili ulitiwa saini mwaka 2014 na kuanzisha operesheni Barkhane ili kuisaidia Mali kupambana na makundi ya kigaidi.

Nchi ya Mali imekuwa ikisumbuliwa na uasi na machafuko ya ndani tangu mwaka 2012, licha ya uwepo wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa (MINUSMA) na wanajeshi wa Ufaransa waliotumwa nchini humo katikati ya mwaka 2013 kwa shabaha ya kurejesha amani na utulivu nchini humo.