Jan 25, 2022 07:53 UTC
  • Wakazi wa Beni DRC waandamana wakitaka kuondolewa mzingiro

Mtu mmoja ameuawa huku wengine 30 wakikamatwa na maafisa usalama katika maandamano ya wakazi wa mji wa Beni wanaoshinikiza kuondolewa 'hali ya mzingiro' katika majimbo ya kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yaliyokumbwa na machafuko na mauaji ya mara kwa mara ya magenge ya waasi.

Sebastien Kahuma, kamisha mkuu wa polisi katika mji wa Beni amesema maandamano hayo ya jana yaligeuka na kuwa ya fujo, huku baadhi ya waandamanaji wakivamia maduka na mabenki.

Amesema polisi walilazimika kutumia nguvu kukabiliana na waandamanaji baada ya makundi ya vijana  miongoni mwa waandamanaji kufunga barabara kuu zinazoelekea katika jiji hilo la kaskazini mwa nchi.

Polisi ya DRC imesema vijana hao walichoma moto pikipiki mbili katika barabara ya Kanzuli Beni-Mangina, na kwamba mtu mmoja ameuawa kwa kupigwa risasi na maafisa usalama.

Wakazi wa Beni wakiandamana kushinikiza kuondoka askari MONUSCO

Mei mwaka jana, Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo alitoa amri kwa jeshi na polisi wa nchi hiyo kuchukua jukumu la kuendesha mzingiro katika majimbo hayo ya kaskazini mwa nchi.

Licha ya serikali ya DRC kutangaza hali ya mzingiro katika mikoa hiyo ya Ituri na Kivu Kaskazini, lakini mauaji ya raia yangali yanashuhidiwa. Ongezeko la mashambulizi ya magenge yenye silaha na machafuko ya kikabila yamesababisha vifo vya mamia ya watu huku wanajeshi wa serikali na walinda amani wa Umoja wa Mataifa (MONUSCO) wakijaribu kuleta utulivu mashariki mwa nchi hiyo bila mafanikio.

Tags