Jan 25, 2022 07:59 UTC
  • Makumi ya watu wauawa katika mapigano ya kikabila Sudan Kusini

Watu wasiopungua 30 wameuawa huku wengine wengi wakijeruhiwa katika mapigano ya kikabila nchini Sudan Kusini.

Duru za habari ziliripoti habari hiyo jana Jumatatu na kuongeza kuwa, watu 33 wakiwemo watoto wadogo wameuawa katika mapigano hayo ya kikabila katika jimbo la Jonglei, mashariki mwa Sudan Kusini.

Matuor Mabior, Katibu Mkuu wa Chama cha Vijana wa Jamii ya Bor alinukuliwa na shirika la habari la Anadolu jana Jumatatu akisema kuwa, vijana wa kabila la Pibor mwishoni mwa wiki walivamia eneo la Baidit Payam katika jimbo la Jonglei, na kutekeleza mauaji hayo.

Amesema idadi kubwa ya mifugo ya wakazi wa eneo hilo imeibiwa katika uvamizi huo, akisisitiza kuwa hali ya taharuki ingali imetanda katika eneo hilo.

Ramani ya Sudan Kusini

Naye Kamishna wa Kaunti ya Bor Kusini, Yuot Alier amethibitisha kutokea shambulio hilo la Jumapili, akieleza kuwa watu 20 wamejeruhiwa, huku nyumba nyingi zikichomwa moto.

Mapigano ya wenyewe kwa wenyewe katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika yamepelekea watu zaidi ya 400,000 kuuawa, mbali na mamlioni kufurushwa kwenye makazi yao na kuwa wakimbizi katika kipindi cha miaka saba iliyopita.

 

Tags