Jan 25, 2022 12:15 UTC
  • Algeria yawaonya raia wake kuhusu hatari ya ujasusi wa Israel

Maafisa wa Algeria wametuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa raia wakiwataka kuwa waangalifu na jumbe zinazotia shaka kwa sababu ya uwezekano wa simu zao za rununu kunafanyiwa ujasusi kupitia programu ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa mujibu wa gazeti la Al-Shorouk, hatua hiyo imechukuliwa sambamba na habari kwamba Algeria na raia wake wamekuwa wakilengwa kwa programu ya kijasusi ya Israel, Pegasus, inayotumiwa na watawala wa Morocco, wakiwemo viongozi, wazee, wamiliki wa ardhi, viongozi wa makabila, wanajeshi wa ngazi za juu, wakurugenzi, wakuu wa usalama na maafisa wengine wa utendaji.

Tahadhari hiyo ya ujumbe wa maandishi imetolewa kwa raia wa Algeria baada ya gazeti la Israel la Haaretz kuchapisha orodha ya wahanga wa programu ya kijasusi ya Israel inayojulikana kwa jina la Pegasus, wakiwemo wanahabari, wanaharakati wa kisiasa na wanasheria wa Kiarabu.

Programu ya Pegasus inatumiwa kufanya ujasusi nchini Algeria

Vyombo vya habari vya dunia, likiwemo gazeti la Ufaransa Le Monde, hivi karibuni vilichapisha uchunguzi uliofanywa na taasisi mbili za sheria za kimataifa ambao unaonyesha kuwa maelfu ya simu za rununu nchini Algeria zinaweza kuwa shabaha za programu ya kijasusi ya Pegasus ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika miezi ya karibuni Algeria imekuwa mstari wa mbele kukabiliana na njama za utawala wa Kizayuni wa Israel na kuwatetea Wapalestina wanaoendelea kukandamizwa na kuuawa na utawala huo.