Jan 26, 2022 07:29 UTC
  • Rais Kagame ayataka mataifa ya Afrika kushirikiana zaidi katika ulinzi wa anga

Rais Paul Kagame wa Rwanda ameyataka mataifa ya Afrika kuwa na ushirikiano zaidi katika sekta ya ulinzi wa anga wakati huu hali ya usalama ikiripotiwa kudorora katika baadhi ya mataifa ya Kiafrika.

Rais Kagame ambaye nchi yake ina vikosi vya kulinda amani kwenye mataifai kadhaa ya Kiafrika ameyasema hayo mjini Kigali mji mkuu wa Rwanda alipokuwa akihutubia kwenye ufunguzi wa mkutano wa siku nne wa wakuu wa majeshi ya anga kutoka nchi 30 za Afrika.

Mkutano huo unafanyika kwa ushirikiano na kikosi cha anga cha Marekani katika nchi za Kiafrika na Ulaya na lengo ni kutathmini ushirikiano unaoendelea baina ya jeshi la anga la Marekani katika nchi za Afrika na Ulaya kwa ajili ya kukabiliana na visa vinavyohatarisha usalama katika kanda ya nchi hizo.

Askari wa Rwanda wa kusimamia amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati wakiwa katika doria

 

Wakuu wa majeshi ya anga kutoka nchi hizo 30 kila mmoja atapata nafasi ya kufafanua changamoto zinazolikabili jeshi lake na mikakati inayochukuliwa kuhakikisha usalama wa kimkakati unafikiwa. Katika ufunguzi wa kikao hicho ambacho kinafanyika wakati dunia ikikabiliwa na virus hatari vya corona imesemekana kwamba hakuna nchi hata moja ambayo bila ushirikiano na nchi nyingine inaweza kutimiza ndoto ya usalama endelevu.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake katika ufunguzi wa mkutano huo, Rais Kagame amesema, usalama na amani ni msingi wa maendeleo endelevu kwa kila nchi, hivyo kuimarisha usalama huo si jambo ambalo linawezekana pasi na kuweko ushirikiano baina ya mataifa ya dunia.