Jan 26, 2022 07:30 UTC
  • Watu 32 wauawa katika mapigano ya makabila hasimu Sudan Kusini

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, kwa akali watu 32 wameuawa katika mapigano baina ya makabila hasimu katika nchi ya Sudan Kusini.

Mapigano hayo yametokea katika jimbo la Jonglei na kwamba, wanawake na watoto ni miongoni mwa waliouawa katika mapigano hayo huku watu wasiopungua 26 wakiripotiwa kujeruhiwa.

Timu ya Kusimamia Amani ya Umoja wa Mataifa sambamba na kulaani vikali mapigano na mauaji hayo, imeitaka serikali ya Juba kuwasaka na kuwatia mbaroni wale wote waliohusika na mauaji hayo.

Sudan Kusini imekuwa ikiandamwa na jinamizi na vurugu na machafuko huku serikali ya Juba ikishindwa kukabiliana na makundi yanayobeba silaha ambayo yamehatariisha amani na usalama kwa wananchi wa nchi hiyo.

Moja ya makundi ya wabeba silaha Sudan Kusini

 

Nchi hiyo changa zaidi barani Afrika ilitumbukia kwenye machafuko na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe mwezi Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kumtuhumu makamu wake wakati huo, Riek Machar kuwa alipanga njama ya kumpindua.

Sudan Kusini ambayo miaka kumi iliyopita ilijitenga na Sudan na kujitangazia uhuru, ingali inakabiliwa na matatizo mengi kama ukosefu wa usalama na amani huku asilimia kubwa ya wananchi wa nchi hiyo wakiishi chini ya mstari wa umasikini licha ya taifa lao kuwa na utajiri wa mafuta.

Ukosefu wa usalama na amani umesababisha maelfu kwa maelfu ya raia wa Sudan Kusini kuyakimbia makazi yao.

Tags