Jan 26, 2022 11:25 UTC
  • Mapinduzi ya Burkina Faso na mustakbali usiojulikana wa nchi hiyo

Kundi la askari wa jeshi la Burkina Faso linalojiita Patriotic Movement for Safeguarding and Restoration chini ya uongozi wa Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba Jumatatu wiki hii lilijitokeza katika tevisheni ya taifa ya nchi hiyo likitangaza kusitishwa Katiba, kuivunja Serikali na Bunge na kumuondoa madarakani Rais wa nchi hiyo, Roch Marc Christian Kabore. Wanajeshi hao walisema kuwa Burkina Faso sasa iko chini ya mamlaka yao.

Taarifa hiyo ya wanajeshi walofanya mapinduzi iliyosainiwa na kiongozi wao. Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba ambayo ilisomwa kwa wananchi kupitia televisheni ya taifa imedai kuwa, jeshi limechukua mamlaka ya nchi bila ya machafuko na umwagaji damu na kwamba viongozi wa serikali waliotiwa nguvuni wako mahala salama. Taarifa ya wanajeshi waliofanya mapinduzi Burkina Faso imeongeza kuwa, sababu iliyopelekea kukamatwa Rais wa nchi hiyo ni kutokana na kuongezeka ukosefu wa usalama ndani ya nchi na kushindwa kwake kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi hiyo. 

Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba, kiongozi wa mapinduzi Burkina Faso 

Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba ni kati ya makamanda wa ngazi ya juu wa jeshi aliyehudumu na kupambana kwa miaka kadhaa dhidi ya magaidi wenye mielekeo ya kufurutu ada. Mapinduzi ya Burkina Faso yalitokea siku moja baada ya vikosi vya jeshi la nchi hiyo  kuanzisha uasi katika baadhi ya kambi zao ambapo sauti za milioni ya risasi ziliripotiwa pia katika mji mkuu wa nchi hiyo, Ouagadougou. Itakumbukwa kuwa, wiki moja kabla ya mapinduzi haya, wanajeshi 11 walitiwa mbaroni wakituhumiwa kula njama ya kumpindua Kaboré. Aidha duru za kiusalama huko Burkina Faso zilitangaza kuwa Rais Kabore, Spika wa Bunge na mawaziri wa serikali wanashikiliwa na wanajeshi katika kambi yao kwenye mji mkuu wa nchi hiyo Ouagadougou.   

Nchi mbalimbali duniani zimelaani mapinduzi hayo ya Burkina Faso ukiwemo Umoja wa Mataifa ambao umetaka kuachiwa huru Rais wa Burkina Faso. Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) pia zimelaani mapinduzi ya Burkina Faso na kulitaka jeshi la nchi hiyo kurejea katika majukumu yake ya awali ya kulinda usalama. Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) pia zimetoa taarifa tofauti zikitaka kuachiwa huru haraka iwezekanavyo Rais Roch Marc Christian Kaboré wa Burkina Faso.

Rais Roch Marc Christian Kaboréwa Burkina Faso aliyepinduliwa na jeshi 

Inaonekana kuwa sababu zaidi iliyowasukuma wanajeshi wa Burkina Faso kufanya mapinduzi na kumtia nguvuni rais wa nchi hiyo ni kushindwa kwake kupambana ipasavyo na magaidi wenye misimamo mikali ambao kwa miaka kadhaa sasa wameifanya nchi hiyo kuwa kituo cha kuendeshea mashambulizi na hujuma zao. Hujuma na mashambulizi ya makundi ya kigaidi ya kitakfiri huko Burkina Faso kwa karibu miaka saba sasa yamepelekea kuuliwa raia wa Burkina Faso zaidi ya elfu mbili na wengine milioni moja na nusu pia wamelazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi. Kikosi kilichoasi ndani ya jeshi la Burkina Faso ambacho kinaongoza nchi kwa sasa Jumapili iliyopita kiliagiza kufutwa kazi wakuu mbalimbali wa jeshi na kutengwa fedha zaidi na misaada ya kilojistiki kwa lengo la kupambana na magaidi wenye mfungamano na kundi la Daesh na mtandao wa al Qaida.  

Taarifa ya kikosi cha wanajeshi wafanya mapinduzi imeashiria waziwazi kuwa, Rais Kabore ameshindwa kuwaunganisha wananchi wa Burkina Faso na kushughulikia ipasavyo ukosefu wa usalama ambao unatishia misingi yote ya nchi hiyo. Burkina Faso imekuwa ikitatizwa na mashambulizi ya wanamgambo wenye silaha tokea mwaka 2015. Mashambulizi hayo yalipamba moto mwezi Novemba mwaka jana ambapo watu 53 waliuawa na magaidi hao, aghalabu yao wakiwa ni askari usalama. Kuhusu harakati za makundi ya kigaidi barani Afrika, Jordan Koop ambaye ni mchambuzi wa masuala ya siasa anasema: Katika siku za usoni kutajiri vita halisi dhidi ya ugaidi barani Afrika. Uasi wa pili wa makundi yenye kufurutu ada Magharibi mwa Afrika unazijumuisha Mali, Burkina Faso na Niger.  

Matatizo ya kiusalama yanayofanana na yale yaliyoisibu Burkina Faso yalisababisha mapinduzi ya jeshi katika jirani ya Mali mwezi Mei mwaka jana. Mwezi Septemba mwaka uliopita wa 2021 pia kulifanyika mapinduzi nchini Guinea Conakry.

Burkina Faso ni nchi ya tatu sasa huko magharibi mwa Afrika ambayo katika miaka ya karibuni imekumbwa na mapinduzi ya wanajeshi. Nchi mbili yaani Guinea Conakry na Mali tayari zimewekewa vikwazo vya jumuiya ya ECOWAS ili kurejesha demokrasia na utawala wa katiba. Inatazamiwa kuwa Ecowas itaichukulia Burkina Faso hatua sawa na zile ilizoziwekea nchi za Guinea Conakry na Mali iwapo wanajeshi hawataachia madaraka ya nchi.

Tags