Jan 26, 2022 12:07 UTC
  • Watu 12 wauawa katika hujuma za wanamgambo wa ADF nchini DRC

Watu wasiopungua 12 wameuawa katika mkoa wa Ituri, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kufuatia mashambulio ya waasi wa Uganda wa ADF.

Wanaharakati wa haki za binadamu wamesema hayo leo Jumatano na kuongeza kuwa, wapiganaji wanaosadikika kuwa wa ADF wameshambulia vijiji vya Mutuheyi na Mapendo mkoani Ituri na kufanya mauaji hayo ya kikatili.

Christophe Munyanderu, mkuu wa asasi moja ya haki za binadamu mkoani Ituri amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, wanamgambo hao walivishambulia vijiji hivyo wakitokea mkoa jirani wa Kivu Kaskazini.

Kwa mujibu wa mwanaharakati huyo, idadi ya waliouawa katika mashambulio hayo ya usiku wa kuamkia Jumatatu ni watu 13, mbali na kuchomwa moto nyumba sita na pikipiki nne.

Msemaji wa Jeshi la DRC, Jules Ngongo Tshikudi amethibitisha kushambuliwa vijiji hivyo viwili katika mkoa wa Ituri, lakini hajatoa idadi ya waliouawa na kujeruhiwa katika hujuma hizo.

Maafisa usalama mkoani Ituri

Kundi hilo la waasi linalotokea kaskazini mashariki mwa Uganda limekuwa likiendesha shughuli zake katika maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa DRC tangu muongo wa 90, ambapo limeua mamia ya watu, na kupelekea malaki ya wengine kuwa wakimbizi. 

Hujuma hizo zimefanyika katika hali ambayo, tokea Mei 6 mwaka jana hadi sasa, Rais Felix Tshisekedi wa DRC ameiweka chini ya hali ya mzingiro mikoa ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.  

Tags