Jan 26, 2022 12:13 UTC
  • Kimbunga 'Ana' chaua watu 34 Madagascar, 2 Msumbiji

Makumi ya watu wameaga dunia kutokana na kimbunga kikali kilichoipiga Madagascar kwa siku kadhaa sasa.

Idara ya kukabiliana na maafa ya kimaumbile ya Madagascar ilitangaza hayo jana Jumanne na kuongeza kuwa, watu 34 wamepoteza maisha kutokana na kimbunga hicho.

Kimbunga hicho cha kitropiki kwa jina la Ana ambacho kilitua Madagascar wiki iliyopita, kimepelekea watu zaidi ya 65,000 kusalia bila ya makazi katika kisiwa hicho kilichoko katika Bahari ya Hindi, kusini mashariki mwa bara la Afrika.

Madagascar imekuwa ikikumbwa na vimbunga mara kwa mara ambavyo mbali na kusababisha maafa na kupelekea malaki ya watu kuachwa bila makazi, lakini huathiri pia miundomsingi na mifumo ya mawasiliano.

Wakati huohuo, watu wawili wamefariki dunia kutokana na kimbunga hicho huko Msumbiji. Kimbunga hicho kimesababisha upepo mkali na mvua kubwa katika wilaya za katikati na kaskazini mwa nchi.

Mchoro wa ramani inayoonesha kimbunga kinavyosafiri kwa kasi

Idara ya Kitaifa ya Kupambana na Majanga ya Msumbiji imesema kimbunga hicho kimesababisha watu karibu 50 kujeruhiwa vibaya katika mkoa wa Zambezia, mbali na maelfu ya wengine kupoteza makazi yao.

Katika nchi jirani ya Malawi, kimbunga hicho kimesababisha mvua, maporomoko ya ardhi na mafuriko yaliyopelekea kukatika kwa huduma za umeme katika baadhi ya maeneo ya nchi.

Tags