Jan 26, 2022 12:16 UTC
  • Jeshi la Somalia lakomboa miji, vijiji 10 vilivyokuwa vimetwaliwa na al-Shabaab

Jeshi la Taifa la Somalia limefanikiwa kukomboa miji na vijiji kadhaa vya nchi hiyo vilivyokuwa vimetekwa na wapiganaji wa kundi la kigaidi la al-Shabaab.

Duru za kijeshi kutoka Somalia zinaarifu kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo wamefanya operesheni kabambe kusini mwa jimbo la Shabelle ya Kati na kukomboa miji miwili na vijiji vinane vilivyokuwa mikononi mwa al-Shabaab.

Katika operesheni hiyo iliyofanyika katika maeneo ya Hawadley na Jameo, viungani mwa wilaya ya Balad iliyoko umbali wa kilomita 40 kaskazini mwa mji mkuu Mogadishu, wanamgambo 10 wa al-Shabaab wameangamizwa.

Aidha jeshi la Somalia limetwaa silaha na zana za kivita za magaidi hao, sanjari na kuteketeza kikamilifu maficho yao.

Maiti za wanamgambo wa al-Shabaab

Operesheni hiyo ya jana Jumanne imejiri siku moja baada ya wanamgambo wa al-Shabaab kukiri kufanya shambulio la bomu katika mgahawa mmoja ulioko katika mji wa Qalimow, ambapo watu 6 wakiwemo askari 4 waliuawa.

Somalia imekuwa katika vita na mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la al-Shaabab lilioasisiwa mwanzoni mwaka mwaka 2004, na ambalo limetangaza kuwa na mfungamano na mtandao wa al-Qaeda.

Tags