Jan 27, 2022 02:37 UTC
  • Waasi nchini Ethiopia watishia kuanzisha tena mapigano katika eneo la Afar

Waasi wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray wa (TPLF) katika eneo hilo la kaskazini mwa Ethiopia, wamesema wamechokozwa na hivyo wataanzisha operesheni katika jimbo jirani la Afar, hali inayorudisha nyuma matumaini ya kumaliza mzozo huo unaoendelea kwa mwezi wa 14 sasa.

Waasi hao wamesema, wameshambuliwa na wapiganaji wanaoiunga mkono serikali  ya Ethiopia, na kubainisha kuwa wapiganaji haop watiifu kwa serikali ya Addis Ababa wameanzisha hujuma dhidi yao tangu Januari 24.

Hatua hii imekuja baada ya waasi hao wa kundi la TPLF kutangaza kuondoka katika jimbo hilo la Afar na lile la Amhara tangu mwezi mmoja uliopita.

Kuondoka kwao kulileta matumaini ya kurejea amani katika eneo la kaskazini mwa Ethiopia, katika mzozo huo ambao umesababisha vifo vya maelfu ya watu na wengine kukosa huduma muhimu za binadamu kama chakula na dawa.

Abiy Ahmed

Katika hatua nyingine, wafanyakazi wanaohusika na utoaji wa misaada ya kibinadamu wanaendelea kupata changamoto ya kuwafikia waathiriwa wa mgogoro wa eneo la Tigray, huku malori yakizuiwa katika jimbo la Afar.

Vita katika eneo la Tigray vilianza Novemba mwaka 2020 baada ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kuliagiza jeshi lishambulie eneo hilo kufuatia tuhuma alizotoa dhidi ya wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray TPLF kwamba walivishambulia vikosi vya jeshi.../

 

Tags