Jan 27, 2022 03:37 UTC
  • Askari 20 wa DRC wauawa katika mashambulio ya waasi wa M23

Askari zaidi ya 20 wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameuawa katika mashambulio mapya ya kundi la waasi la M23 mashariki mwa nchi.

Duru za habari zinaarifu kuwa, makumi ya wanajeshi wa DRC wameuawa katika makabiliano makali yanayoendelea tokea Jumatatu baina askari hao na wapiganaji wa M23 katika eneo la Nyesisi, karibu na Hifadhi ya Wanyamapori ya Virunga mkoani Kivu Kaskazini.

Gentil Karabukala, mkuu wa shirika moja la kiraia amesema mapigano hayo yaliendelea kushuhudiwa hadi jana Jumatano, na kwamba idadi ya askari waliouawa ni 29.

Nalo shirika la Kivu Security Tracker (KST) linalofuatilia hali ya usalama katika eneo hilo la DRC limesema idadi ya wanajeshi waliouawa katika mashambulio hayo ya M23 ni 26. Waasi wa kundi la M23 walianzisha uasi mwaka 2012 nchini Kongo wakilalamikia kuwepo ufisadi na vitendo viovu ndani ya jeshi la DRC.

Waasi wa M23

Wanaharakati wa haki za binadamu jana Jumatano waliripoti pia habari ya kuuawa raia 12 katika mkoa wa Ituri, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kufuatia mashambulio ya waasi wa Uganda wa ADF.

Hujuma hizo zimefanyika katika hali ambayo, tokea Mei 6 mwaka jana hadi sasa, Rais Felix Tshisekedi wa DRC ameiweka chini ya hali ya mzingiro mikoa ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.  

Tags