Jan 27, 2022 07:49 UTC
  • Watu 19 waaga dunia kutokana na athari za kimbunga 'Ana' Malawi

Idara ya Kitaifa ya Kupambana na Majanga ya Malawi imesema watu 19 wamefariki dunia kutokana na kimbunga kikali cha kitropiki kilichopewa jina la Ana katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo.

Taarifa ya idara hiyo imesema watu 107 wamejeruhiwa, huku wengine 216,972 wakiachwa bila makazi kutokana na taathira hasi za kimbunga hicho katika nchi hiyo ya kusini mashariki mwa Afrika.

Kimbunga hicho kimesababisha mvua, maporomoko ya ardhi na mafuriko yaliyopelekea kukatika kwa huduma za umeme katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

Watu zaidi ya milioni 20 hawana umeme mbali na kusumbuliwa na uhaba wa maji kwa sasa hususan katika miji ya Blantyre, Zomba, Lilongwe na Mzuzu.

Wakati huohuo, kimbunga Ana kimesababisha watu karibu 50 kujeruhiwa vibaya katika mkoa wa Zambezia nchini Msumbiji, mbali na maelfu ya wengine kupoteza makazi yao.

Idara ya kukabiliana na maafa ya kimaumbile ya Madagascar pia ilitangaza juzi Jumanne kuwa, watu 34 wamepoteza maisha kutokana na kimbunga hicho kilichopewa jina la 'Ana.'

Tags