Jan 27, 2022 07:53 UTC
  • Mali yapuuza miito ya Ulaya ya kutaka askari wa Denmark wabaki nchini humo

Mali imesisitiza kuwa Denmark inapaswa kuondoa wanajeshi wake mara moja katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi ambao walitumwa nchini humo kama sehemu ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Ufaransa, licha ya nchi za Ulaya kuiasa iangalie upya msimamo wake huo.

Ufaransa pamoja na nchi nyingine 14 za Ulaya zimesema zimesikitishwa na hatua ya serikali ya Mali ya kutaka kuondoka mara moja nchini humo vikosi maalumu vya Denmark vilivyopo katika eneo la Takuba nchini humo, kama sehemu ya muungano wa kijeshi wa Ufaransa, ulioko nchini humo 'kupambana na magenge ya ugaidi.'

Serikali ya mpito ya Mali hivi karibuni ilieleza kuwa, Denmark imetuma askari wake nchini humo pasi na kuishauri au kuitaarifu serikali ya Bamako, na vile vile hatua hiyo imekiuka Protokali ya Ziada inayozihusu nchi za Ulaya washirika wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Mali inasisitiza kuwa, ombi lililotumwa mwezi Juni mwaka jana na Denmark la kutaka kuruhusiwa kutumwa wanajeshi wake katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi limewekwa pembeni kwa sasa, kama yalivyowekwa maombi ya Norway, Ureno na Hungary.

Askari wa kigeni nchini Mali

Haya yameripotiwa wakati huu ambapo serikali ya Mali pia inapanga kupitia upya mkataba wa ushirikiano wa kijeshi na kiulinzi kati yake na Ufaransa. Mkataba huo kati ya nchi hizo mbili ulitiwa saini mwaka 2014 na kuanzisha operesheni Barkhane ili kuisaidia Mali kupambana na makundi ya kigaidi.

Mali imekuwa ikisumbuliwa na uasi na machafuko ya ndani tangu mwaka 2012, licha ya uwepo wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa (MINUSMA) na wanajeshi wa Ufaransa waliotumwa nchini humo katikati ya mwaka 2013 kwa shabaha ya kurejesha amani na utulivu nchini humo.

Tags