Jan 27, 2022 08:13 UTC
  • ECOWAS yaitisha mkutano wa kujadili mgogoro wa Burkina Faso

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) kesho Ijumaa zitafanya mkutano wa kujadili mgogoro wa kisiasa uliobuka Burkina Faso, kufuatia kujiri mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani Rais Roch Marc Christian Kaboré wa nchi hiyo.

ECOWAS imesema katika taarifa kuwa, mkutano huo wa dharura wa kujadili mapinduzi ya Burkina Faso utafanyika kwa njia ya intaneti, kuanzia majira ya saa nne asubuhi.

Tayari jumuiya hiyo ya kieneo imetoa taarifa ya kulaani mapinduzi hayo, na kulitaka jeshi la nchi hiyo kurejea katika majukumu yake ya awali ya kulinda usalama.

Siku ya Jumatatu, kundi la wanajeshi waliofanya mapinduzi wakiongozwa na Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba, liliibuka na kutoa taarifa kupitia televisheni ya taifa likidai kuwa, jeshi limechukua mamlaka ya nchi bila ya machafuko na umwagaji damu na kwamba viongozi wa serikali waliotiwa nguvuni akiwemo rais wako mahala salama. 

Lilitangaza kusitishwa Katiba, kuivunja Serikali na Bunge na kumuondoa madarakani Rais wa nchi hiyo, Roch Marc Christian Kabore, likisisitiza kuwa Burkina Faso sasa iko chini ya mamlaka yao.

Kundi la wanajeshi waliofanya mapinduzi Burkina Faso

Taarifa ya wanajeshi waliofanya mapinduzi Burkina Faso ilieleza kuwa, sababu iliyopelekea kukamatwa Rais wa nchi hiyo ni kutokana na kuongezeka ukosefu wa usalama ndani ya nchi na kushindwa kwake kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi hiyo. 

Nchi mbalimbali duniani zimelaani mapinduzi hayo ya Burkina Faso ukiwemo Umoja wa Mataifa ambao umetaka kuachiwa huru Rais Kabore. Aidha Umoja wa Afrika (AU), Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) pia zilitoa taarifa tofauti za kulaani mapinduzi hayo.

Tags