Jan 27, 2022 10:22 UTC
  • Askari aliyepindua serikali ya Burkina Faso alipata mafunzo Marekani

Afisa wa kijeshi aliyeoongoza mapinduzi yaliyopelekea kupinduliwa rais aliyechaguliwa kidemokrasia Burkina Faso alipata mafunzo yake Marekani.

Rais Roch March Christian Kaborre alipinduliwa Jumatano na afisa kijana jeshini ambaye alitangaza kusimamisha katiba huku akiivunja serikali. Kinara wa mapinduzi hayo ya kijeshi ambaye sasa ni kiongozi wa Burkina Faso ni  Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba, ambaye alikuwa kiongozi wa moja ya maeneo matatu ya kijeshi nchini humo.

Dambia alipata mafunzo ya kiwango cha juu ya kijeshi kutoka Jeshi la Marekani ambalo lina historia ndefu ya kuwafunza askari ambao wamepindua serikali za kidemokrasia barani Afrika. Dambia alipata mafunzo katika mazoezi kadhaa ya kijeshi ambayo husimamiwa na Kamandi ya Jeshi la Marekani Afrika maarufu kama AFRICOM. Mbali na Dambia, wanajeshi wengine walioongoza mapinduzi ya kijeshi katika nchi za Afrika Magharibi wamepata mafunzo Marekani. Tokea mwaka 2008, maafisa wa kijeshi waliopata mafunzo ya kijeshi Marekani eneo la Afrika Magharibi, huko Guinea, Mali, Mauritani na Gmabia walipata mafunzo Marekani.

Wakati huo huo, nchi wanachama wa Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) kesho Ijumaa zitafanya mkutano wa kujadili mgogoro wa kisiasa uliobuka Burkina Faso, kufuatia kujiri mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani Rais Roch Marc Christian Kaboré wa nchi hiyo.

ECOWAS imesema katika taarifa kuwa, mkutano huo wa dharura wa kujadili mapinduzi ya Burkina Faso utafanyika kwa njia ya intaneti, kuanzia majira ya saa nne asubuhi.

Nchi mbalimbali duniani zimelaani mapinduzi hayo ya Burkina Faso ukiwemo Umoja wa Mataifa ambao umetaka kuachiwa huru Rais Kabore. Aidha Umoja wa Afrika (AU), Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) pia zimetoa taarifa tofauti za kulaani mapinduzi hayo.  

 

Tags