Jan 27, 2022 11:52 UTC
  • Maandamano ya Wasudani kupinga uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya nchi hiyo

Raia wa Sudan wanaendelea kufanya maandamano wakipinga uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya nchi yao na wamemtaka mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuondoka nchini humo.

Mzozo wa kisiasa nchini Sudan ulipamba moto mwezi Oktoba mwaka jana, kufuatia mapinduzi ya jeshi lililonyakua madaraka ya nchi. Ijapokuwa jeshi la Sudan limejaribu kutafuta njia ya kutatua mzozo uliopo hivi sasa kwa kutumia njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kufanya makubaliano na waziri mkuu aliyejiuzulu, Abdallah Hamdok, lakini sera hizo bado hazijafanikiwa. Wananchi wa Sudan wanaamini kuwa, uwepo wa jeshi kwenye usukani wa madaraka ni kinyume na malengo yao yaliyopelekea kuondolewa madarakani rais wa zamani Omar al-Bashir. Wasudani wanataka kuondoka madarakani kikamilifu jeshi la nchi hiyo na kuanzishwa serikali halali na ya kidemokrasia, lakini maafisa wa jeshi hawako tayari kuondoka madarakani.

Suala hili limechochea zaidi maandamano ya wananchi dhidi ya wanajeshi wanaotawala Sudan. Hata hivyo maandamano hayo yamekabiliwa kwa ngumi ya chuma. Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu ya Sudan imetoa taarifa ikitaka kuheshimiwa haki ya kufanya maandamano ya amani na kuwalinda raia wakati wa maandamano. Tume hiyo pia imetoa wito wa kusitishwa ukandamziaji dhidi ya raia. Ripoti ya Jumuiya ya Madaktari wa Sudan inasema, waandamanaji zaidi ya 70 wameuawa kwa kupigwa risasi na jeshi tangu Oktoba 25 mwaka jana.

Wasudani wakipambana na askari usalama

Sambamba na hayo kunashuhudiwa ongezeko la uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya Sudan. Nafasi, rasilimali na utajiri wa Sudan vimeyatia tamaa madola ya kigeni yanayofanya kila liwezekanalo kwa ajili ya kusimika serikali kibaraka na tegemezi. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, mgogoro wa kisiasa wa Sudan umetayarisha uwanja wa madola ya kigeni ukiwemo utawala wa Kizayuni wa Israel kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamekaribisha hatua ya jeshi la Sudan ya kunyakua madaraka ya nchi hiyo. Katika mkondo huo pia wiki iliyopita ujumbe wa Israel uliwasili Khartoum na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Baraza la Utawala wa kijeshi la nchi hiyo, Abdel Fattah al Burhan, licha ya maandamano makubwa ya wananchi.

Hivi karibuni tovuti ya Axios ya Marekani ilitangaza kuwa, kwa muda mrefu sasa Al-Burhan amekuwa mhusika mkuu katika harakati za kutaka kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala unaoikalia Quds kwa mabavu na amekuwa akichukua hatua zake kwa mujibu wa maagizo ya Baraza la Usalama la Israel hususan shirika la ujasusi la utawala huo, Mossad. Tovuti hiyo imeongeza kuwa, Rais Joe Biden wa Marekani amemtuma Waziri wake wa Mambo ya Nje, Antony Blinken aitake Israel itumie uhusiano wake mkubwa na al Burhan na kumshawishi arejeshe utawala wa kiraia nchini Sudan. Suala hili limezidisha hasira za wananchi wa Sudan.

Wasudani wakichoma moto bendera ya Israel

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa mwenye makazi yake London nchini Uingereza, Abdel Bari Atwan anasema: "Urithi adhimu wa taifa la Sudan katika medani ya Kiarabu na Kiislamu unapingana kikamilifu na vitendo vya kufedhehesha vya wanajeshi waliofanya mapinduzi kwa kutumia jina la wanajihadi na wanamapambano wa Sudan. Katika vipindi vyote wananchi hao wamekuwa kigezo cha ubinadamu, kujitolea, kufa shahidi, kupigania uadilifu na kutetea malengo ya Umma wa Kiislamu, na harakati hii ya sasa ya wananchi itaendelea hadi wahusika wa hali ya sasa ya Sudan na watu wake watakapofikishwa mahakamani."

Kwa sasa wananchi wa Sudan wanataka kurejeshwa madarakani serikali ya kiraia na kidemokrasia na kukomeshwa uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya nchi yao.   

Tags