Jan 28, 2022 06:31 UTC
  • Wanajeshi wasiopungua 33 wa serikali wameuawa kaskazini mashariki mwa DRC

Wanajeshi wasiopungua 33 wameuawa katika mapigano yaliyozuka baina ya wanajeshi wa serikali na waasi wa M23 kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mapigano yamepamba moto tangu siku ya Jumanne katika eneo la Rutshuru la kaskazini mwa mji wa Goma ambayo ni makao makuu ya mkoa wa Kivu Kaskazini, ambapo pia mapigano yanaendelea baina ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrsia ya Congo (FARDC) na waasi wa M23.

Taarifa ya kuuawa wanajeshi 33 wa serikali akiwemo mwanajeshi mwenye cheo cha kanali na kamanda wa moja ya vikosi vya jeshi hilo imetolewa katika hali ambayo, jana Alkhamisi kulitangazwa habari ya kuua wanajeshi 20 wa serikali baada ya kushambuliwa na waasi wa M23 mashariki mwa nchi hiyo. 

Waasi wa M23

 

Taarifa hiyo ya jana ilisema kuwa, makumi ya wanajeshi wa DRC wameuawa katika mapigano makali yanayoendelea tokea Jumatatu baina askari hao na waasi wa M23 katika eneo la Nyesisi, karibu na Hifadhi ya Wanyamapori ya Virunga mkoani Kivu Kaskazini.

Gentil Karabukala, mkuu wa shirika moja la kiraia amesema mapigano hayo yaliendelea kushuhudiwa hadi Jumatano, na kwamba idadi ya askari waliouawa ni 29.

Kundi la M23 ni la waasi wa National Congress for the Defense of the People (CNDP). Tarehe 23 Machi, 2009 kundi hilo lilifikia makubaliano na serikali ya Congo, lakini viongozi wa M23 wanadai kuwa serikali ya DRC haiheshimu makubaliano yaliyofikiwa baina ya pande mbili.