Jan 28, 2022 10:19 UTC
  • Mwanajeshi aliyefanya mapinduzi Burkina Faso azungumza kwa mara ya kwanza

Kamanda aliyeongoza mapinduzi ya kijeshi nchini Burkina Faso, kwa mara ya kwanza amezungumza na wananchi tangu baada ya kufanya mapinduzi hayo na kuahidi kuirejesha nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, katika mfumo imara wa demokrasia ya kuheshimiwa Katiba.

Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba amesema katika hotuba yake hiyo ya kwanza kwa wananchi kwamba, Burkina Faso itarejea katika mfumo wake wa zamani wa kuheshimu Katiba, ingawa hakutangaza tarehe hasa ya kufanyika jambo hilo. 

Matamshi hayo yamekuja baada ya viongozi wa vyama vya upinzani nchini Burkina Faso kutoa taarifa rasmi ya kuunga mkono mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini humo tarehe 24 mwezi huu wa Januari na ambayo yamemng'oa madarakani Rais Roch Marc Christian Kabore.

Vyama vya upinzani nchini Burkina Faso vikitangaza kuunga mkono mapinduzi ya kijeshi nchini humo

 

Katika taarifa yao ya jana Alkhamisi, wapinzani hao wamesema, migogoro na matatizo mengi yaliyoikumba Burkina Faso kama vile ukosefu mkubwa wa usalama, mgogoro wa uchumi na matatizo mengine mengi kwenye sekta za jamii tangu mwaka 2015 yametokana na uzembe na udhaifu wa serikali iliyokuwepo madarakani.

Sehemu nyingine ya taarifa ya vyama hivyo vya upinzani imesema, vikosi vya ulinzi vimelazimika kuingilia masuala ya siasa nchini Burkina Faso kama sehemu ya kulinda usalama wa taifa hata kama mapinduzi ya kijeshi katika nchi ya kidemokrasia na ya utawala wa wananchi, kimsingi hayakubaliki.

Kabla ya kutolewa taarifa hiyo ya wapinzani ya kuunga mkono mapinduzi ya kijeshi nchini Burkina Faso, wanajeshi waliofanya mapinduzi hayo walikuwa wamewatahadharisha mawaziri wa serikli iliyoong'olewa madarakani wasitoke nje ya mji mkuu wa nchi hiyo Ouagadougou hasa wakati huu wa mazungumzo yanayojadili namna Burkina Faso inavyoweza kurejea katika uchaguzi wa kidemokrasia.