Jan 28, 2022 10:28 UTC
  • Watu 6 wafa maji na 30 hawajulikani walipo baada ya boti kuzama karibu na Tunisia

Watu wasiopungua 6 kutoka nchi mbalimbali za Afrika wamekufa maji na wengine 30 hawajulikani walipo baada ya wahamiaji hao haramu kujaribu kuvuka Bahari ya Mediterranean kuelekea barani Ulaya.

Wizara ya Ulinzi wa Tunisia imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, gadi ya ufukweni ya Tunisia imeopoa miili sita ya wahamiaji hao na kuokoa wengine 34. Hadi inaripotiwa habari hii, gadi hiyo ya ulinzi wa ufukweni ya Tunisia ilikuwa inaendelea na zoezi la kutafuta watu wengine waliokuwemo kwenye boti hiyo. Taarifa ya wizara hiyo imewanukuu watu waliokolewa kwenye ajali hiyo wakisema kuwa, boti hiyo ilikuwa na watu 70 na walikuwa wanaelekea nchini Italia kupitia Bahari ya Mediterranean na kwamba boti hiyo haikutokea nchini Tunisia.

Kwa mujibu wa manusura hao, boti hiyo ilikuwa inatokea nchini Libya na ilizama umbali wa kilomita 40 kutoka kwenye fukwe za mji wa Zarzis wa Tunisia ambao uko karibu na mpaka wa Libya. Mkuu wa shirika la Msabala Mwekundu la nchini Tunisia, Mongi Slim, amesema, watu waliokoloewa ni raia wa nchi za Kiafrika za Misri, Sudan na Icory Coast.

Wahamiaji haramu wanaishi katika mazingira magumu kaskazini mwa Afrika

 

Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa limetangaza kuwa, karibu wahajiri haramu 60,000 waliwasili nchini Italia mwaka jana 2021 lakini zaidi ya watu 1,200 walipoteza maisha wakati walipojaribu kuvuka bahari yenye mawimbi makali kuelekea Italia mwaka huo. 

Wizara ya Ulinzi wa Tunisia imesema kuwa, mamlaka husika zimezuia safari 8 za wahamiaji haramu katika kipindi cha masaa 48 yaliyopita katika mji wa ufukweni wa Sfax. Watu 130 wametiwa mbaroni katika kipindi hicho cha masaa 48, wengi wao wakiwa ni raia wa Tunisia na wengine ni kutoka nchi za chini ya jangwa la Sahara.