Jan 28, 2022 10:31 UTC
  • Afrika CDC: Tuna malengo ya kupiga chanjo asilimia 70 ya wakazi wa bara la Afrika mwaka huu

Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Afrika CDC kimesema kuwa, kina malengo ya kupiga chanjo asilimia 70 ya wakazi wa bara hilo hadi mwishoni mwa mwaka huu wa 2022 kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa wa UVIKO-19 au corona.

Mkurugenzi wa Afrika CDC, John Nkengasong ametoa taarifa hiyo na kuongeza kuwa, hivi sasa karibu asilimia 11 ya wakazi bilioni 1.3 wa bara la Afrika wameshapata chanjo kamili ya corona na kwamba lengo hilo la kuwapiga chanjo asilimia 70 ya wakazi wa bara hilo linaweza kufikiwa mwishoni wa mwaka huu.

Amesema, kasi ya kupiga chanjo katika nchi kama Nigeria imekipa matumaini kituo hicho ya kuweza kufikia malengo yake ya kupiga chanjo asilimia 70 ya wakazi wa bara la Afrika ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2022.

 

 

Amesema, utafiti na uchunguzi wa maoni ukiwemo ule uliofanywa na kituo chake unaonesha kuwa asilimia 80 ya watu wa nchi zilizofanyiwa utafiti na kukusanywa maoni ya wananchi, wamesema wako tayari kupiga chanjo kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa wa corona. 

Pamoja na hayo lakini amesema, kila yanapotokea makelele kuhusu chanjo kama vile kupita muda wake au tatizo la nchanjo kama za AstraZeneca kutofika kwa wakati unaotakiwa, mambo hayo huzusha wasiwasi na kupunguza mwamko wa kupiga chanjo barani Afrika.

Kituo hicho cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Afrika CDC pia kimesema, nchi za Afrika hadi hivi sasa zimeshapokea dozi milioni 580 za UVIKO-19 na asilimia 64 ya dozi hizo zimeshatumika.