Jan 29, 2022 02:57 UTC
  • Waathirika wa kimbunga nchini Msumbiji wapokea msaada wa UN

Zaidi ya watu 45,000 wakiwemo wanawake na watoto 23,000, huenda wakahitaji msaada wa kibinadamu baada ya kimbunga kupiga majimbo ya Nampula, Zambezia, Tete, Niassa, Sofala na Manica nchini Msumbiji.

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto UNICEF limepeleka wafanyakazi na kuandaa vifaa vya matibabu na lishe, maji, vyoo, vifaa vya usafi, pamoja na kutenga maeneo ya kujifunzia kwa watoto na familia zilizoathiriwa na kimbunga Ana.

Kimbunga hicho kilichoikumba nchi ya Msumbiji mnamo Januari 24 kilisababisha mafuriko na kuharibu takriban nyumba 10,500 pamoja na miundombinu ya umma ambayo ni madaraja, shule, vituo vya afya, nyaya za umeme na mifumo ya maji.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Kitaifa ya Kupunguza na Kudhibiti Maafa ya Msumbiji (INGD), hadi kufikia Januari 26, vituo vya afya 12 na vyumba vya madarasa 346 ( katika shule 137) vimeharibiwa na kuwaacha wanafunzi 27,383 bila mahali pa kujifunzia ikiwa ni wiki moja tu kabla ya kuanza muhula mpya wa masomo Jumatatu tarehe 31 Januari. Takwimu hizi zinatarajiwa kuongezeka wakati tathmini ikiendelea kufanyika.

Picha ya satalaiti ya kimbunga Ana kikiwa nchini Msumbiji Januari 24 2022

UNICEF inakadiria kuwa itahitaji dola za Marekani milioni 3.5 ili kukabiliana na mahitaji ya haraka ya watu walioathiriwa na Kimbunga Ana na tayari imeanza kutumia vifaa vyake vilivyonunuliwa awali huku ikiendelea na uchangishaji fedha kwa wadau wa ndani.

Kuanzia 2016 hadi 2021, Msumbiji imekabiliwa na matukio mawili ya ukame na vimbunga ikiwa ni pamoja na Cyclones Idai na Kenneth ambayo ilipiga nchi hiyo mwaka 2019 na ndani ya muda wa wiki sita na kuathiri watu milioni 2.5.

Kulingana na chombo cha kutathmini hatari ya maafa INFORM, Msumbiji inashika nafasi ya 9 kati ya nchi 191 duniani kutokana na tishio kubwa la nchi hiyo kukumbwa na hatari, kukabiliwa na hatari, na ukosefu wa uwezo wa kukabiliana nayo.