Jan 29, 2022 08:10 UTC
  • ECOWAS yasimamisha uanachama wa Burkina Faso kufuatia mapinduzi ya kijeshi

Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS imesimamisha uanachama wa Burkina Faso baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini humo na kuifanya nchi ya tatu mwanachama, mbali na Guinea na Mali kupewa adhabu hiyo ndani ya kipindi cha miezi 18, kwa sababu ya wanajeshi kunyakua madaraka katika nchi hizo.

Tangazo hilo la kusimamishwa uanachama wa Burkina Faso limetolewa siku kadhaa baada ya wanajeshi waasi kumlazimisha ajiuzulu rais Roch Marc Christian Kabore ambaye amechaguliwa kidemokrasia.

Watawala wapya wa kijeshi nchini Burkina Faso wametetea uamuzi wao wa kufanya mapinbduzi kwa kudai kwamba rais Kabore ameshindwa kuzima machafuko ambayo yamepelekea maelfu ya watu kuuawa wakati wa utawala wake.

Rais Nana Addo Dankwa Akufo-Addo wa Ghana ambaye ndiye mwenyekiti wa sasa wa ECOWAS na ambaye ndiye aliyeongoza kikao cha viongozi wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo kilichofanyika jana kwa njia ya intaneti ili kujadili mapinduzi ya kijeshi ya Burkina Faso amesema, mapinduzi kadhaa ya kijeshi ambayo yamefanyika hivi karibuni katika mataifa ya Afrika Magharibi ni ukiukaji wa moja kwa moja wa misingi na thamani za kidemokrasia.

Akufo-Addo ameongeza kuwa, dunia inawatazama wao ikiwategemea kuchukua msimamo thabiti juu ya suala hilo.

Luteni Kanali Paul-henri Tamiba,

Ujumbe wa wakuu wa majeshi ya nchi wanachama wa ECOWAS unatazamiwa kuelekea mji mkuu wa Burkina Faso Ouagadougou leo Jumamosi ili kukutana naye na kujaribu kumshinikiza kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi Luteni Kanali Paul-henri Tamiba, na utafuatiwa na wa ngazi ya mawaziri utakaoelekea nchini humo siku ya Jumatatu.

Viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magahribi watakutana Februari 3 katika mji mku wa Ghana, Accra ili kutathmini matokeo ya kazi itakayofanywa na jumbe zitakazotumwa nchini Burkina Faso na kuona kama nchi hiyo iwekewe vikwazo pia mbali na kusimamishwa uanachama wake.../